Samia: Sekta binafsi itakuwa nguzo ya utendaji wa Serikali

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa Serikali ya awamu ya sita katika muhula wake wa pili itaendeleza mageuzi ya kiuchumi kwa kuipa kipaumbele sekta binafsi, kuwekeza zaidi katika kilimo na kuimarisha huduma za afya.

 Akizungumza leo Ijumaa, Novemba 14, 2025, wakati wa kulifungua Bunge la 13 jijini Dodoma, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuitambua sekta hiyo kama mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Katika kufanikisha ukuaji wa sekta binafsi, amesema Serikali itaboresha mazingira ya biashara kwa kukamilisha utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara.

Sambamba na hilo, ameahidi kutekeleza mapendekezo ya tume aliyoiunda ya kuboresha mifumo ya kodi nchini, ili kuwapatia wafanyabiashara wepesi katika kufanya biashara zao.

Amesema hilo litakwenda sambamba na kuweka nguvu zaidi katika kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa, hatua ambayo ni muhimu katika kupunguza gharama za maisha ya wananchi.

“Pia tutaweka motisha kwa viwanda vya ndani ili vizalishe kwa gharama nafuu na kuuza kwenye soko la ndani na nje. Tutaenda kuondoa vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi ili kuchochea uzalishaji na kukuza ushindani wa bidhaa za ndani,” amesema Rais huyo.

Katika kuhakikisha ustawi wa vijana, amesema Serikali itafungua fursa mahususi za kuhamasisha vijana na wamiliki wa biashara ndogondogo kupata elimu ya biashara.

Vilevile, amesema atawawezesha vijana kujisajili kwenye mfumo wa manunuzi wa kielektroniki wa Serikali.

Kupitia vyuo vya ufundi stadi, Rais Samia amesema wataongeza programu maalumu za mafunzo ya ufundi stadi na kuziunganisha na miradi ya kimkakati kama reli ya kisasa, uendelezaji wa bandari, uchumi wa buluu, madini na gesi ili vijana wapate uzoefu na kuajirika.

Amesema Serikali itaanzisha kanda za kuendeleza ujuzi zitakazowezesha vijana kupata ujuzi unaohitajika katika kampuni za sekta binafsi na kuangalia uwezekano wa kutoa vivutio maalumu kwa kampuni zitakazotoa nafasi nyingi za ajira kwa vijana.

“Pia, tutaweka mazingira ya kuhakikisha tunakuza vijana kwenye uongozi kwa kuwezesha vyuo vyetu kufanya mafunzo ya ulezi (mentorship) na ukuzaji wa vijana viongozi. Matamanio yangu ni kuona ifikapo 2030 tuwe tumetengeneza wawekezaji vijana ambao watatoa ajira kwa vijana wenzao,” amesema.

Katika sekta ya kilimo, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye sekta hiyo, akisema itaongozwa na dhana ya ‘kilimo ni biashara, mkulima ni mwekezaji.’

Lengo la kufanya hivyo, amesema ni kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta hiyo kutoka asilimia nne ya sasa hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

“Kwa kufanya hivyo, tunalenga sio tu kujihakikishia utoshelevu wa chakula, bali pia tutawekeza kwenye mnyororo wa thamani, ili kuwanufaisha Watanzania wengi walioajiriwa kwenye sekta hii,” amesema Rais Samia.

Amesema anakusudia kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya mahindi, mchele na mbogamboga barani Afrika.

Rais Samia amesema anafanya hivyo, kwa kujielekeza kwenye kilimo cha kisasa kwa kuongeza pembejeo kama mbegu bora, mbolea na viuatilifu kwa ruzuku.

Pia amesema wataongeza upatikanaji wa maji ya uhakika na kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka ekari milioni 3.4 hadi ekari milioni tano.

Utekelezwaji wa hilo, Rais Samia amesema utafikiwa kwa kukamilisha ujenzi wa mabwawa na skimu za umwagiliaji zinazoendelea na kuanzisha mpya kwenye Bonde la Mto Rufiji.

Aidha, amesema Serikali itaanzisha pia vituo vya ukodishaji zana za kilimo, vitakavyotoa huduma za matumizi ya teknolojia katika kilimo.

“Ili kukuza uwekezaji kwenye sekta ya kilimo, tutaziimarisha benki zetu za Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Benki ya Ushirika ili zichochee mapinduzi tunayoyatazamia,” amesema.

Katika hotuba yake hiyo, amesema tangu aingie madarakani katika muhula huu siku 12 zilizopita, tayari ameshatangaza nafasi za ajira 7,000 za walimu na 5,000 za watumishi wa afya.

Hatua hiyo amesema ni mwanzo wa kujibu kiu ya wananchi ya kuboresha huduma za afya na elimu.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali inajiandaa kuanza majaribio ya Bima ya Afya kwa Wote, huku akiwataka wabunge kupokea mapendekezo ya namna ya kufanikisha majaribio hayo.

“Tunadhamiria pia kuviunganisha vituo vya huduma za afya kidijitali na kuhakikisha vinakuwa na vifaa na huduma za viwango stahiki kwa kila ngazi husika,” amesema.

Amesema anakusudia kuweka viwango vinavyofanana ili watumiaji wa bima ya afya mijini na vijijini wawe na huduma zinazolingana.

Wakati huohuo, Rais huyo amesema ameshaielekeza Wizara ya Afya kusimamia maelekezo ya kutozuiwa maiti kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, wakati familia zikiendelea na taratibu za kulipa deni la matibabu kwa njia zinazolinda utu wao.

Amewasihi wananchi wote kuweka kipaumbele kwa afya zao, kwa kila mmoja kuwa na bima ya afya pamoja na wanaomtegemea.