Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania kama Taifa linapenda liheshimiwe kama linavyoheshimu mataifa mengine na katika kulinda masilahi ya nchi, hakuna mbadala.
Amesema lazima kuhakikisha tunalinda utu, uhuru, na heshima ya Taifa letu na kwamba nchi itaendelea kuongozwa kwa misingi ya sera ya nje iliyoasisiwa na waasisi ya kutofungamana na upande wowote.
Rais Samia ametoa msimamo huo leo, Ijumaa Novemba 14, 2025 alipozungumza katika hotuba yake ya kulifungua Bunge la 13, jijini Dodoma.
“Msimamo wetu ni umoja na ushirikiano badala ya mgawanyiko, majadiliano badala ya amri au mabavu na haki badala ya visasi,” amesema.
Amesema Tanzania imejengwa katika misingi ya amani na utulivu wa kisiasa na haitakubali nguvu yoyote inayokusudia kuchafua misingi hiyo.
Ametumia jukwaa hilo kuweka wazi kuwa Serikali yake itaendelea kuviimarisha vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha mipaka na raia wanalindwa vema.
Amesema Tanzania itaendelea kutimiza wajibu wake wa kuchangia misheni za ulinzi wa amani za kikanda na kimataifa.
“Msingi wa mafanikio ya yote haya ni utawala wa sheria, uadilifu na uwajibikaji kuanzia juu hadi chini. Kufanikiwa kwa yote tuliyoyasema ni kuwa na misingi imara kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za nchi pamoja na kupata huduma wanazostahili,” amesema.
Amesema Serikali yake itaelekeza jitihada zake kwenye mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, ubadhilifu, uzembe, ukosefu wa nidhamu na maadili.
Amesema lazima wachache wanaotaka kuirudisha nchi kwa kuendekeza masilahi binafsi wadhibitiwe.
Ili kuimarisha uwajibikaji serikalini, amesema ataendeleza kutekeleza programu za maboresho ya utumishi wa umma ikiwemo matumizi ya mifumo ya upimaji wa utendaji kazi.
“Wajibu huendana na haki na haki huendana na wajibu. Hivyo, pamoja na kuwataka watumishi wawajibike, tutaendelea kuboresha masilahi yao kwa kadri uchumi utakavyoruhusu,” amesema.
Ameeleza Serikali yake itaimarisha uwajibikaji na utendaji wa mashirika ya umma, ili kuboresha ufanisi, uwazi na tija na anachotaka kuongeza sio tu gawio bali kuchangia angalau asilimia 10 ya mapato yote.