KIKOSI cha Singida Black Stars kimeingia kambini jana kujiandaa na maandalizi ya mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CR Belouizdad, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela huko Algiers Novemba 22.
Mechi hiyo ya kundi C ilipangwa kuchezwa Jumapili ya Novemba 23, ila imerudishwa nyuma na sasa itachezwa Jumamosi ya Novemba 22, ambapo kikosi hicho kimeingia kambini, baada ya pambano la Ligi Kuu dhidi ya Pamba Jiji, Novemba 8, 2025.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida, Hussein Massanza, amesema baada ya mechi ya mwisho na Pamba iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, wachezaji walipewa mapumziko ya siku nne, ila Novemba 12, wameingia kambini kujiandaa na safari ya Algeria.
“Wachezaji wako katika hali nzuri kwa mujibu wa daktari wa timu, Khalid Aucho alipata majeraha madogo lakini kwa sasa anaendelea vizuri, benchi la ufundi halikumtumia mechi na Pamba ili kumpa muda zaidi mzuri wa kupona,” amesema Massanza.
Aidha, Massanza amesema licha ya kocha mkuu wa kikosi hicho, Miguel Gamondi kuendelea na majukumu yake ya timu ya Taifa ya Taifa Stars, ila ameacha programu maalumu kwa wasaidizi wake, ambao wataendelea kuzifanyia kazi kwa muda asiokuwepo.
Massanza amesema kikosi hicho kitaweka kambi ya maandalizi ya mechi hiyo na CR Belouizdad jijini Dar es Salaam, na inatarajia kuondoka Novemba 19.