Russia. Leo ni Siku ya Kisukari Duniani, chini ya uratibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) yenye kaulimbiu isemayo “Kisukari na Ustawi.”
Katika kuadhimisha siku hii muhimu, tunajadili kisukari cha aina ya pili kwa watoto, ugonjwa unaoongezeka kwa kasi duniani kote.
Kama ilivyo kwa watu wazima, kisukari cha aina ya pili hutokea pale ambapo mwili hautoi insulini ya kutosha au seli hushindwa kuitumia ipasavyo.
Ni ugonjwa sugu unaoathiri jinsi mwili wa mtoto unavyosindika sukari kwa ajili ya nishati. Bila kudhibitiwa, sukari hukusanyika kwenye damu na kusababisha madhara ya muda mrefu.
Sababu kubwa ya ongezeko la kisukari-2 kwa watoto ni unene kupita kiasi na ulaji usiofaa unaotokana na kutofanya mazoezi ya kutosha pamoja na matumizi ya vyakula vyenye mafuta, sukari na wanga mwingi.
Tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya watoto wenye kisukari aina ya pili wana unene kupita kiasi. Njia rahisi ya kuzuia hali hii ni kudhibiti uzito mapema kupitia lishe bora na kushiriki michezo.
Wataalamu wanapendekeza uchunguzi wa kisukari kwa watoto wenye umri wa miaka 10 au zaidi ambao ni wanene au wazito kupita kiasi, hasa kama wana sababu nyingine za hatari kama vile historia ya familia yenye kisukari.
Dalili kuu za kisukari aina ya pili kwa watoto ni kupata kiu kali, kukojoa mara kwa mara, kuhisi njaa isiyoisha, uchovu, udhaifu, uoni hafifu, kupungua uzito ghafla na kupata maambukizi ya mara kwa mara.
Chanzo halisi cha ugonjwa huu hakijulikani, lakini kuna mambo kadhaa yanayoongeza uwezekano wa mtoto kupata kisukari-2.
Miongoni mwao ni unene na mafuta mengi tumboni yanayosababisha seli kuwa sugu kwa insulini. Kutofanya mazoezi ya mara kwa mara pia huongeza hatari ya kupata ugonjwa huu.
Ulaji wa vyakula visivyo na uwiano mzuri wa virutubishi kama nyama nyekundu, vyakula vilivyosindikwa, vinywaji vyenye sukari na mafuta ni sababu nyingine muhimu.
Aidha, mtoto mwenye mzazi au ndugu aliye na kisukari yuko katika hatari kubwa kutokana na urithi wa kinasaba.
Utafiti unaonyesha kuwa baadhi ya makundi ya watu, wakiwamo watu weusi, Wahispania, Wahindi wa Amerika na Waasia wa Amerika, wako kwenye hatari kubwa zaidi, ingawa bado haijulikani kwa nini tofauti hii ipo.
Kisukari-2 pia hujitokeza zaidi wakati wa ujana, hasa kwa wasichana, ingawa kinaweza kumpata mtoto katika umri wowote. Watoto waliozaliwa na mama waliokuwa na kisukari cha ujauzito wako katika hatari kubwa zaidi, sambamba na wale waliozaliwa wakiwa na uzito mdogo au kabla ya muda kamili wa ujauzito.
Ili kuwalinda watoto dhidi ya tatizo hili, mazoezi ya mara kwa mara na michezo ni muhimu kuanzia ngazi ya familia hadi shuleni.
Ni vyema kuwahimiza watoto kushiriki michezo ya jadi na shughuli zinazohusisha viungo vyote vya mwili. Wazazi na walezi wanapaswa pia kuwaelimisha watoto kuhusu madhara ya ulaji holela wa vyakula vyenye sukari, wanga na mafuta mengi, hasa vile vyenye asili ya kimagharibi.
Kisukari cha aina ya pili hakina tiba kamili, lakini kinaweza kuzuilika kwa kubadili mtindo wa maisha.
Ni jukumu letu sote wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kusaidia watoto wetu kukua wakiwa na afya njema na ustawi bora.