Vibonge Kunyimwa Visa? Haya Ndiyo Mapya Kutoka Serikali ya Rais Trump – Global Publishers



Serikali ya Rais Donald Trump inakusudia kuanza kuwanyima visa wahamiaji wa kigeni wenye unene uliopitiliza (vibonge).

Inaelezwa kuwa mbali na unene uliopitiliza, wahamiaji wengine wenye changamoto za kiafya ambazo zinaweza kuleta mzigo wa ziada kwa serikali, wanaweza kukataliwa maombi ya visa.

Waraka uliotumwa kwa balozi mbalimbali za Marekani duniani umewataka maafisa wa utoaji wa visa “kuzingatia afya ya mwombaji,” na kuongeza kuwa unene uliopitiliza unaweza kusababisha magonjwa kama pumu, shinikizo la damu na maradhi mengine ambayo yanaigharimu serikali.

Waraka huo uliendelea kueleza kuwa magonjwa ya moyo na mishipa, magonjwa ya kupumua, saratani, kisukari, magonjwa ya mfumo wa mwili kuchakata chakula (metabolic diseases), magonjwa ya neva, na matatizo ya afya ya akili pia yanapaswa kuzingatiwa.

“Hali hizo zinaweza kuhitaji huduma zenye thamani ya mamia ya maelfu ya dola na huduma pana na za muda mrefu,” unasema waraka huo uliotiwa saini na KFF Health News.