Vigezo vilivyombeba Nchemba kuwa Waziri Mkuu

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema uteuzi wa Dk Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania umepitia ushindani mkubwa na vigezo kadhaa, akiwashinda wenzake kwa sifa.

Amesema Dk Mwigulu amefanya kazi katika sekta ya fedha kwa muda mrefu na anazijua chochoro za upatikanaji wa rasilimali hiyo, akitarajia atamsimamia Waziri wa Fedha atakayeteuliwa kufanya kazi hiyo.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Ijumaa, Novemba 14, 2025, alipohutubia baada ya kumuapisha Dk Mwigulu kushika wadhifa huo, hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma.

“Vigezo vyote vilivyopimwa, tumepima katika maeneo mbalimbali ya kuitumikia nchi hii na kulitumikia Taifa hili. Kubwa zaidi ni kuwatumikia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.

Amesema uteuzi wa Dk Mwigulu umepitia ushindani mkubwa na katika vigezo kadhaa ameibuka na sifa nyingi zaidi kuwazidi wengine alioshindana nao.


Amesema, pamoja na kazi zake kuwa katika Katiba, pia amemkabidhi vitabu vya maelekezo ya kazi zinazopaswa kufanywa naye.

Samia amesema Dk Mwigulu anapokea kijiti kutoka kwa mfanyakazi mzuri na kwamba hana shaka atafuata nyayo zake na kuongeza pale panapohitaji kuongezwa.

Dk Mwigulu amepokea kijiti kutoka kwa Kassim Majaliwa, aliyeshika wadhifa huo kwa miaka 10, akianzia utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya hayati Dk John Magufuli.

Katika hotuba hiyo, Samia amesema, kama alivyoahidi wakati wa kampeni na kama Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025/30 ilivyoahidi, kunahitajika kasi ya utekelezaji wa yaliyopangwa iongezwe ili yatimizwe ndani ya muda mfupi.

“Utekelezaji wa kazi zote hizo unahitaji fedha, na wewe umetoka katika sekta ya fedha, kwa muda wa miaka mitano umejua chochoro vyote tulivyokuwa tukipita kutafuta fedha,” amesema, na kuongeza:

“Kwa hiyo utamsimamia atakayekaa kwenye nafasi yako (Wizara ya Fedha), ili naye aweze kupita kule tulikopita, fedha ipatikane na kazi ifanyike. Kwa kifupi, una kazi kubwa sana.”

Samia amemweleza kuwa kazi aliyompa ni ngumu hasa kwa umri wake (wa miaka 50), kwa kuwa anakumbana na vishawishi vya ndugu, jamaa na marafiki, akimtaka ahakikishe anafanya kazi ya kulitumikia Taifa.


“Mengine uliyasema mwenyewe jana (Novemba 13) ulipokuwa bungeni nilikusikiliza vizuri, ni imani yangu kwamba hukuyasema tu, lakini una moyo wa dhati wa kuyasimamia,” amesema.

Rais Samia amesema: “Tukutakie kazi njema, mzigo huu si mdogo, na kwa umri wako, sijui Kassim aliingia akiwa na umri gani, mzigo huu ni mkubwa, kwa umri wako vishawishi ni vingi vya marafiki, ndugu, jamaa na wengine. Nafasi yako ile haina rafiki, ndugu wala jamaa, ni nafasi ya kulitumikia Taifa hili.”

Baada ya kuteuliwa na kuthibitishwa na Bunge jana, Novemba 13, kwa kura 369 kati ya 371 zilizopigwa huku mbili zikiharibika, Dk Mwigulu ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi alitoa onyo kwa watumishi wazembe na waliotoa rushwa.

“Watumishi wavivu, wazembe na waliotoa rushwa nakuja na fyekeo na rato, lazima kila mmoja awajibike na tutekeleze ahadi alizozitoa Rais Samia Suluhu Hassan. Watumishi na Watanzania wote lazima twende na gia ya kupandia mlima, cha msingi ni kuwa chombo kifike salama,” alisema.


Aliahidi katika uongozi wake atahakikisha watumishi wa umma wanatenga muda wa kuwasikiliza wananchi, na inapobidi lazima waondoke ofisini ili kutatua kero za watu.

“Watanzania wa mazingira ya chini watasikilizwa kwa nidhamu katika ofisi za umma. Tutahakikisha watumishi wanakwenda kutatua kero za wananchi katika maeneo yao. Hata hivyo, Dira ya Taifa ya Maendeleo imebeba matumaini makubwa ya Watanzania na kazi ni kubwa, twendeni tukaisimamie,” alisema.