Dar es Salaam. Uwepo wa wanawake katika nafasi za uongozi pekee hakutoshi katika uwezeshaji wa wanawake, bali fursa hiyo inapaswa kuambatana na nguvu ya kufanya uamuzi.
Vilevile, ushiriki wa wanaume katika safari ya kuwawezesha wanawake nao umetajwa kama jambo muhimu kwa kuwa wote wanategemeana.
Msisitizo umetolewa kuwa, haiwezekani kufikia malengo ya uwezeshaji wa wanawake bila kuwajumuisha wanaume.
Hayo yameelezwa kwenye mkutano wa uongozi wa wanawake, ulioandaliwa na Women Leadership in Insurance Africa (WLIAfrica) Tanzania, uliofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 14, 2025 ukiwa na kaulimbiu: “Tumewezeshwa kuongoza, wanawake wataitengeneza kesho.
Mkurugenzi Mkazi wa WLIAfrica, Lora Mbwette, amesema wameandaa mkutano huo baada ya kubaini wanawake wanapokuwa kwenye uongozi wanakosa nguvu ya kufanya uamuzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications,RosalynnMndolwa-Mworia akizungumza katika Mkutano wa uongozi wa wanawake ulioandaliwa na Women Leadership in Insuarance Africa (WLIAFRICA),jijini Dar es Salaam.Picha na Michael Matemanga
“Tunajua zipo jitihada za kuwafanya wanawake kuwa viongozi, sasa jitihada tunazofanya ni kuwafanya wengi wawe katika eneo la kufanya uamuzi,” amesema.
Amesema wanawake kuwa kwenye uongozi hakutoshi, bali wanapaswa kuwa sehemu ya kujadili sera na kuweka mikakati kwa mustakabali wa Taifa la sasa na baadaye.
“Kuwezesha wanawake si kuwapatia fursa pekee za uongozi, bali kuwezesha sauti zao zilete matokeo katika taasisi na mashirika,” amesema.
Amesema kwa Tanzania, wanawake wanashikilia asilimia 37 ya viti vya Bunge, lakini ni asilimia 28 tu ya nafasi za uongozi wa juu na wa kati katika sekta binafsi, sekta ya umma na asasi za kiraia (NGOs) zinazoongozwa na wanawake.
“Wanawake wanawakilisha zaidi ya asilimia 50 ya wajasiriamali, wakionyesha ubunifu na ustahimilivu wa hali ya juu. Hata hivyo, nguvu hii ya ujasiriamali haiakisi mara zote uwezo wa kushiriki katika nafasi za uamuzi,” amesema na kuongeza:
“Takwimu hizi zinaweka wazi jambo moja, uwakilishi pekee hautoshi, wanawake wanazidi kuwapo katika maeneo ya uongozi, lakini ushiriki wao katika nafasi za kufanya uamuzi bado ni mdogo.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Rosalynn Mndolwa-Mworia, aliyekuwa mgeni maalumu katika mkutano huo, amesema wanawake wanapokutana kwenye mikutano ya aina hiyo hawakusudii kuigawai jamii, bali kuponya, kusikiliza na kufikiria kwa upana.
“Kwa hiyo, tunapozungumza kuhusu ushirikiano wa wanawake, tukumbuke daima kuwa wanaume waliokuwa sehemu ya safari yetu ni washirika wetu,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications,RosalynnMndolwa-Mworia akizungumza katika Mkutano wa uongozi wa wanawake ulioandaliwa na Women Leadership in Insuarance Africa (WLIAFRICA),jijini Dar es Salaam.Picha na Michael Matemanga
Amesisitiza umuhimu wa mtu kuzingatia malengo yake, ambayo huanza kwa kutambua kuwa kila hatua anayopitia iwe rahisi au yenye changamoto ni sehemu ya taswira ya maisha.
“Huenda una ndoto zipo ndani yako au unapitia kipindi kigumu, lakini hakuna kinachopotea. Kila jukumu, kila changamoto, kila ushindi mdogo unakuandaa kwa mahali unapokusudiwa kufika,” amesema.
Amesema ushiriki wa wanaume katika safari ya kuwawezesha wanawake ni jambo muhimu kwa sababu wanawake na wanaume wanategemeana.
Kwa upande wake, Mshauri na Mtaalamu wa Uongozi, Omar Kashera, akiwasilisha mada ya namna ya kuzungumza kwenye hadhara, amesema hilo ni tatizo linaloathiri wengi kwenye jamii.
“Watu hawana ujasiri wa kuzungumza mbele ya hadhara, unaweza kuwa na ujumbe muhimu wa kuwasilisha kwa watu lakini unashindwa kuongea mbele yao,” amesema na kuongeza:
“Unapokuwa na ujumbe mzuri, usikae nao mwenyewe na njia nzuri ya kuufikisha ujumbe huo ni kuzungumza. Sasa ni muhimu ukawa na maarifa ya kuwasilisha ujumbe wako.”
Kashera amesema katika mazungumzo hayo ni lazima mtu afahamu anaongea na kundi gani ili kuepusha mkanganyiko wa taarifa kupelekwa eneo lisilo sahihi.
Amesema ili mtu awe mzungumzaji mzuri ni lazima asome vitabu na kupata maarifa mengi yatakayomsaidia kujenga ufahamu wa kile anachotaka kuzungumza.