Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu Watanzania 34 kulipa faini ya Sh40,000, kila mmoja au kwenda jela miezi sita, baada ya kukiri shtaka la kuondoka ndani ya Tanzania na kwenda Afrika Kusini bila kufuata taratibu za uhamiaji.
Waliohukumiwa adhabu hiyo katika kesi ya jinai namba 27040 ya mwaka 2025 ni Abilah Mpili, Abdallah Abdallah, Idrisa Lwambo, Rajab Fundi, Halid Kondopembe na wenzao 29.
Hata hivyo, washtakiwa hao wamefanikiwa kulipa faini na kukwepa adhabu ya kwenda kutumikia kifungo cha miezi sita jela.
Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa Novemba 14, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, baada ya washtakiwa kukiri kosa lao na mahakama kuwatia hatiani kwa kosa hilo.
Hakimu Nyaki amesema washtakiwa wametiwa hatiani kama walivyoshtakiwa na wamekiri wenyewe shtaka lao.
“Nimezingatia washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na wote mmeomba msamaha mbele ya mahakama hii, hivyo ninawahukumu kila mmoja kulipa faini ya Sh40,000 na mkishindwa mtatumikia kifungo cha miezi sita jela” amesema Hakimu Nyaki na kuongeza
” Haki ya kukata rufaa ipo wazi iwapo hamjaridhika na adhabu hiyo.”
Awali, akiwasomea hoja za awali, Wakili wa Mohamed Mlumba akishirikiana na Ezekiel Kibona alidai kuwa washtakiwa waliondoka nchini bila kufuata taratibu wa uhamiaji wa kutoka na kuingia nchini.
Alidai washtakiwa hao walikwenda Afrika Kusini kinyume cha sheria.
Mlumba alidai kati ya mwaka 2000 hadi Juni 2025, washtakiwa waliondoka nchini kwenda Afrika Kusini kupitia mipaka tofauti bila kuwa na hati ya kusafiria.
Washtakiwa hao walirudishwa nchini Novemba 11, 2025 wakitoka Afrika Kusini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere( JNIA) uliopo wilaya ya Ilala, na kisha walipelekwa ofisi za uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa kwa njia ya maelezo.
Wakiwa ofisi za Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam, washtakiwa hao walikiri shtaka lao.
Na leo, baada ya kuwasomea maelezo yao, washtakiwa wote walikiri shtaka lao linalowakabili na ndipo walipotia hatiani na kuhukumiwa.
“Mheshimiwa hakimu, upande wa mashtaka hauna kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya washtakiwa hao, ila tunaomba mahakama iwape adhabu kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa vijana wengine wanaokwenda nje ya nchi bila utaratibu” alisema Wakili Mlumba.
Kwa upande wao washtakiwa, waliomba mahakama iwapunguzie adhabu kwani ni kosa lao la kwanza na hawatarudia tena.
Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza shufaa za washtakiwa hao aliwahukumu kila mmoja kulipa faini ya Sh40,000 na wakishindwa wanatakiwa kutumikia kifungo cha miezi sita jela.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kukamatwa Novemba 11, 2025 katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ( JNIA), uliopo wilaya ya Ilala.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa walikuwa wametoka isivyo halali katika ardhi ya Tanzania bila kibali na kueleleka nchini Afrika Kusini.