Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wapongezwa kwa kujituma na kufanya kazi kwa bidii hali iliyopelekea mafanikio makubwa ya Wakala huo ikiwamo kufikisha umeme katika Vijiji vyote vya Tanzania Bara.
Pongezi hizo zimetolewa leo Novemba 14, 2025 na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Nishati, Bi. Ziana Mlawa wakati wa Kikao cha Pili cha Baraza la Wafanyakazi REA liliyofanyika katika ofisi za Wakala huo Jijini Dodoma.
“Sisi pale wizarani tunasema Wizara ya Nishati ni Umeme. Tunaona mnavyofanya kazi kwa bidii. Tupo tayari kushirikiana wakati wote, ili kuhakikisha mnafikia malengo yenu vizuri,”amesema Bi. Ziana
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Wakala wa Nishati vijijini (REA) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Hassan Saidy, amesema mafanikio yaliyofikiwa na REA ni matokeo ya kufanya kazi kwa ushirikiano na bidii huku akiwataka watumishi kuendeleza umoja na kufanya kazi kwa bidii.
Akibainisha baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa ni pamoja na ongezeko la upatikanaji na uunganishaji umeme ambapo upatikanaji wa umeme umeongezeka kutoka asilimia 69.6 mpaka 78.1 kwa maeneo ya vijijini, huku kwa nchi nzima ukiongezeka kutoka asilimia 78.4 mpaka 85.5.
Mhandisi Saidy ameongeza kuwa, kwa upande wa uungaji wa umeme umeongezeka utoka asilimia24.5 mpaka 37.1 kwa maeneo ya vijijini.
Aidha, kwa upande wa matumizi ya nishati safi ya kupikia umeongezeka kutoka asilimia 8 mpaka 23.
“Sisi tuna amini REA imechangia ongezeko la matumizi ya nishati safi ya kupikia. Matumaini ya Watanzania hasa wale wanaoishi vijijini yapo kwetu sisi Wakala wa Nishati Vijijini. Tukafanye kazi kwa bidi kuwahudumia wananchi,” amesisitiza Mhandisi Saidy.
Mwakilishi Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Taifa, Jonas Rwegoshora amesisitiza watumishi wa REA kuwa sehemu ya mabadiliko ya mafanikio ya taasisi hiyo na kuhimiza ushirikiano wa watumishi wote kuanzia ngazi ya chini mpaka juu.


