HATIMAYE amekubali mambo yaishe. Ndiyo, kipa namba moja wa Simba, Moussa Camara amenyoosha mikono na kusitisha mgomo aliokuwa nao, akimalizana na mabosi wa klabu hiyo kwa kukubali kwenda kufanyiwa upasuaji wa goti lake utakaofanyika nje ya nchi.
Camara alikuwa hataki kufanyiwa upasuaji tangu afanyiwe vipimo vya goti lake, kisha madaktari kupendekeza tatizo lake linahitaji ‘kupigwa kisu’ ili aweze kuwa sawasawa, lakini haikuwa rahisi kukubaliana na uamuzi huo.
Taarifa rasmi kutoka Simba ni baada kipa huyo kukubali kufanyiwa upasuaji, klabu hiyo ilimtafuta daktari bora wa kumaliza tatizo la kipa huyo na sasa atapelekwa Morocco kufanyiwa upasuaji huo.
Awali mabosi walikuwa na pendekezo la kipa huyo kutatuliwa tatizo hilo la goti hapa hapa nchini kwa mtaalamu na waliamini wangemfanyia kisasa bila upasuaji, lakini kwa hali aliyonayo Camara wameridhia aende kutibiwa Morocco.
Licha ya Simba kumtafuta daktari huyo, Camara mwenyewe alijiridhisha daktari huyo ni muafaka kumaliza tatizo hilo kufuatia ushauri wa wachezaji wenzake ambao wamewahi kutibiwa na mtaalam huyo.
“Haikuwa rahisi unajua ni muda sasa tulikuwa tunapambana naye akubaliane na hatua ya kufanyiwa upasuaji, lakini hatimaye sasa amekubali atakwenda kufanyiwa hayo matibabu, ilikuwa huwezi kumlazimisha kwa kuwa matibabu ya namna hii ni lazima ipatikane ridhaa ya mgonjwa mwenyewe,” alisema mmoja wa mabosi wa Simba na kuongeza;
“Tulishamtafuta hadi daktari atakayemaliza hili tatizo na bahati nzuri mwenyewe amejiridhisha kwa njia zake ni daktari muafaka. Kumbe kuna wachezaji wenzake wamemhakikishia daktari huyu ni mjuzi wa kumaliza matatizo ya goti kule Morocco.
Aidha bosi huyo aliongeza kwa mujibu wa taarifa ya daktari huyo ni kwamba kipa huyo raia wa Guinea atakuwa nje ya uwanja kwa wiki nane hadi 10 ambayo ni sawa na miezi miwili kuuguza jeraha hilo kisha kurudi uwanjani.
Muda huo ambao Camara atakuwa nje Simba italazimika kubaki na makipa wawili pekee Yakoub Suleiman anayedaka kwa sasa tangu kuumia kwa raia huyo wa Guinea na Hussein Abel ambaye hapati sana muda wa kucheza.
Camara ndani ya muda huo atakosa jumla ya mechi sita za mashindano yote, zikiwemo mechi tatu za Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji na Tanzania Prisons za ugenini pamoja na ile ya nyumbani dhidi ya Yanga, pia akikosa tatu za Ligi ya Mabingwa dhidi ya Petro Atletico, Stade Malien na Esperance de Tunis.