Dar es Salaam. Wakati maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) yakiongezeka kwa kasi na kugeuka chanzo cha mateso hususani kwa wanawake, wataalamu wa afya wanasema tatizo hilo linaweza kuzuiwa kwa kufuata kanuni za afya pasipo ulazima wa tiba.
Tafiti zinaonyesha mwanamke mmoja kati ya wawili nchini Uingereza hupata maambukizi hayo angalau mara moja katika maisha yake, huku zaidi ya theluthi moja wakipata maambukizi ya kujirudia rudia ambayo huathiri usingizi, huleta haja ndogo za mara kwa mara na kusababisha maumivu makali ya tumbo au mgongo.
Wanaume pia hawako salama. Takribani asilimia 12 hupata UTI angalau mara moja maishani na hatari huongezeka maradufu wanapofikisha umri wa miaka 70.
Kwa kawaida, matibabu ya UTI hutegemea dawa za antibiotiki, lakini wataalamu wanasema idadi kubwa ya wagonjwa huendelea kuteseka kwa maambukizi sugu yasiyopona hata baada ya kutumia dawa.
Inaelezwa zaidi ya asilimia 85 ya UTI husababishwa na bakteria kutoka kwenye utumbo au ukeni.
Maambukizi haya hutokea pale bakteria hatarishi, kama E. coli, wanapopenya kutoka nje ya mwili kuingia kwenye njia ya mkojo.
Bakteria hao wanaweza kuathiri njia hiyo (urethra), kibofu cha mkojo au hata figo na kusababisha uvimbe, maumivu na madhara makubwa kama uharibifu wa figo.
Kwa mujibu wa watafiti, kuongezeka kwa maambukizi haya kunachangiwa pia na usugu wa bakteria dhidi ya antibiotiki, hali inayofanya dawa kutofanya kazi ipasavyo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na njia ya mkojo, Sushma Srikrishna, Novemba 9, 2025 alinukuliwa na mtandao wa Daily Mail, nchini Uingereza akieleza njia sita zinazoweza kutumika kujikinga na maambukizi ya UTI, miongoni mwa hizo ni unywaji wa maji ya kutosha.
“Kunywa maji ya kutosha ni msingi muhimu wa kuzuia UTI. Angalau glasi sita hadi nane za maji kwa siku zinahitajika ili kusaidia kusafisha njia ya mkojo na kuondoa bakteria kabla hawajazaliana,” anasema.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Miami na kuchapishwa na jarida la kitabibu la Marekani (Jama) mwaka 2018, unaunga mkono dhana hiyo, ukionyesha wanawake waliokunywa maji zaidi walipata UTI kwa kiasi kidogo kulinganisha na waliokuwa machache.
Dk Srikrishna anashauri wanawake kwenda haja ndogo ndani ya dakika 30 baada ya kujamiiana, ili kuzuia bakteria kuingia njia ya mkojo.
“Kukojoa baada ya tendo husaidia kuwatoa bakteria kabla hawajapanda juu kwenye kibofu,” anasema.
Pia anashauri kuepuka tendo hilo kinyume cha maumbile, akieleza bakteria wa sehemu ya haja kubwa wako karibu na njia ya mkojo, hivyo huongeza hatari ya maambukizi.
Anasisitiza kudumishwa usafi akieleza: “Baada ya kujisaidia jifute kutoka mbele kwenda nyuma.”
Kufanya hivyo anasema husaidia kuzuia bakteria kutoka sehemu ya haja kubwa kuhamia kwenye njia ya mkojo.
Anashauri wanawake kuepuka matumizi ya sabuni zenye manukato makali au poda kwa kuwa zinaweza kuvuruga usawa wa bakteria wa asili wa uke.
Badala yake, anashauri kutumika bidhaa zisizo na harufu na kuvaa chupi za pamba zisizobana ili kuruhusu hewa kupita vizuri.
Anashauri kuepuka matumizi ya vyakula na vinywaji ambavyo husababisha figo kufanya kazi zaidi kwani huiweka katika hatari ya maambukizi.
Anavitaja vinywaji na vyakula hivyo kuwa ni pamoja na vyenye kafeini, pombe, vyenye viungo vikali, matunda na juisi yenye asidi nyingi pamoja na vyakula vyenye sukari iliyoongezwa isiyo ya asili.
“Ingawa vitu hivi havisababishi maambukizi ya UTI moja kwa moja, vinaweza kudhoofisha ulinzi wa asili wa kibofu. Ikiwa wewe ni mtu unayepatwa na UTI mara kwa mara, zingatia kupunguza ulaji wa vitu hivi na kufuatilia kama unagundua uhusiano wowote na dalili zako,” anasema.
Dk Srikrishna anasema kwa wale wanaotumia virutubisho kama kinga ya UTI, ni muhimu kutumia vile vyenye bakteria rafiki wanaolinda mwili dhidi ya magonjwa, hasa kwenye utumbo na mfumo wa mkojo.
“Hii husaidia kuzuia bakteria wabaya kukua na kusababisha maambukizi,” anasema.
Pia anasema ni muhimu kutumia tiba ya homoni ya kike (oestrogen) kwa wanawake waliokoma hedhi, akieleza uzalishaji wake kwao hushuka, hivyo kusababisha ukavu na udhaifu wa tishu za uke.
Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kwa mwanaume, Dk Erasto Wambura anaungana na Dk Srikrishna akisema maumbile ya mwanamke yanamweka katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya UTI kwa haraka, hivyo hatua alizozitaja ni sahihi katika kinga ya hali ya juu.
“Amezingatia tafiti nyingi za hivi karibuni. Mwanamke yupo hatarini zaidi kwa kuwa njia ya mkojo na haja kubwa zimekaribiana, hii ni tofauti na mwanaume ambaye njia yake ya mkojo ni ndefu,” amesema na kuongeza:
“Hatua za kinga ni muhimu zaidi kuzingatia hasa unywaji maji ya kutosha, kufuata hatua alizozitaja baada na wakati wa tendo la ndoa na hatua za kuchukua wakati wa kukoma kwa hedhi,” anasema.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Living Colman pia anasema unywaji wa maji mengi ni kinga bora zaidi, akisisitiza usafi kwa wanawake.
Dk Srikrishna anasema UTI isiyo sugu inaweza kuisha yenyewe, lakini mara nyingi huhitajika antibiotiki.
Anasema pasipo matibabu, maambukizi yanaweza kuenea hadi kwenye figo na kusababisha matatizo makubwa zaidi.
Dalili kuu za UTI ni maumivu au muwasho wakati wa haja ndogo, kukojoa mara kwa mara, mkojo wenye damu, maumivu ya nyonga au mgongo eneo la chini na homa.
Ikiwa mgonjwa ana homa kali, maumivu makali upande mmoja wa mgongo, kichefuchefu, kutapika au kuchanganyikiwa, anasema anashauriwa kutafuta matibabu ya haraka kwani inaweza kuwa ishara ya maambukizi ya figo.
“Kama dalili zinarudi hata baada ya kumaliza dozi ya dawa, daktari anaweza kupendekeza kipimo cha mkojo kubaini aina ya bakteria na dawa sahihi zaidi,” anasema Dk Srikrishna.