Dereva TFS matatani kwa tuhuma za kifo cha bodaboda aliyepakia mkaa

Morogoro. Jeshi la polisi Mkoa wa Morogoro limeanza kuchunguza tukio la ajali ya gari inayodaiwa kuwa ni mali ya wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) ambayo imemgonga na kumsababishia kifo mwendesha pikipiki aliyetambuliwa kwa jina la Edmund Temba (39) mkazi wa Tubuyu, Manispaa ya Morogoro ambaye alikuwa amebeba mkaa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama kupitia taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari ajali hiyo imetokea Novemba 14 majira ya usiku katika eneo la Kipera, Kata ya Mkundi Manispaa ya Morogoro na kuitaja gari inayodaiwa kusababisha ajali hiyo kuwa ni mali ya TFS Mkoa wa Morogoro.

Kamanda Mkama amesema uchunguzi wa awali umebaini dereva anayetuhumiwa kusababisha ajali hiyo ni Nicholaus Simba 38 mkazi wa Manispaa ya Morogoro ambapo alimgonga dereva huyo aliyekuwa akiendesha pikipiki aina ya Haojue.

Aidha kamanda Mkama amesema katika uchunguzi huo wa awali pia wamebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la TFS kushindwa kuchukua tahadhari na kumgonga dereva wa pikipiki na kumsababishia kifo.

“Uchunguzi zaidi kuhusu ajali hiyo na jitihada za kumkamata mtuhumiwa unaendelea, kwa sababu baada ya ajali hiyo dereva huyo alitoroka,” amesema Mkama.

Kufuatia ajali hiyo Kamanda Mkama amewataka madereva wakiwemo wa Serikali kuchukua tahadhari na sheria zote za usalama barabarani ili kulinda maisha ya watumiaji wengine wa barabara.

Akieleza tukio hilo la ajali Mwenyekiti wa Mtaa wa Kipera, Kata ya Mkundi Manispaa ya Morogoro, Bakari Mshana amesema taarifa za ajali hiyo amezipata asubuhi ya leo Novemba 15 kutoka kwa wapitanjia ambao waliona mwili wa mwendesha pikipiki huyo ukiwa kando ya barabara.

“Baada ya kupata taarifa za ajali hii nilikimbilia eneo la tukio na kukuta mwili mwili huo na hivyo nilitoa taarifa kwenye mamlaka husika ambapo saa mbili asubuhi Jeshi la Polisi walikuja kuchukua mwili na kwenda kuhifadhi hospitali,” amesema Mshana.

Amedai, “Huyu dereva wa pikipiki alikuwa na wenzake na walipofika eneo hilo ndipo dereva huyo wa TFS alipoanza kuwakimbiza, mwenzake alifanikiwa kukimbia huyu  naye alikimbilia mashambani na huyu dereva wa TFS alimfuata huko huko na kumgonga.”

Mkazi wa Kipera ambaye alishuhudia mwili huo Francisco Mrando amesema eneo la ajali zilionekana alama ya magurudumu na pikipiki ya marehemu iliyokuwa imebeba kiroba chenye mkaa.

“Huu mwili ulikuwa pembeni mwa barabara na yale magurudumu ya gari yalionekana yamefika mpaka ulipolala mwili, hii inaashiria kuwa huyu dereva alikuwa akimkimbiza dereva wa pikipiki ambaye ni muuza mkaa,” amesema Marando.