Fei Toto avunja ukimya, asema jambo Azam FC

MASHABIKI wa Azam FC walikuwa na hofu kubwa ya kumkosa kiungo mshambuliaji, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyechomolewa timu ya taifa, Taifa Stars kwa sababu ya majeraha, lakini hofu hiyo ni kama inayeyuka baada ya nyota huyo kuvunja ukimya na kuwapa faraja.

Kiungo huyo amewatoa hofu mashabiki wa Azam, kuna uwezekano mkubwa akacheza mechi ya kwanza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS Maniema Union ya DR Congo, ugenini wikiendi ijayo.

Fei ni miongoni mwa  wachezaji wa Stars iliyoitwa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Kuwait inayopigwa leo jijini Cairo Misri, walioshindwa kujiunga na kikosi hicho kutokana na majeraha yanayowakabili, wengine ni Ibrahim Bacca na Mudathir Yahya wa Yanga.

FE 01


Akizungumza na Mwanaspoti, Fei Toto mwenye mabao mawili kwa sasa Ligi Kuu, alisema anaendelea vizuri na karibuni ataanza kufanya mazoezi na wenzake, hivyo mashabiki wasipate hofu kwani anaamini anaweza kabisa kuliwahi pambano la ugenini dhidi ya Maniema.

Fei alisema maendeleo aliyonayo kwa sasa yanampa matumaini ila hatamani kabisa kukosa mechi yoyote ya kimataifa, kwani ana shauku ya kupambania nembo ya Azam iliyoingia kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya michuano ya CAF tangu ianze kuishiriki mwaka 2013.

FE 02


“Niwatoe hofu mashabiki wote wa soka wanaotamani kuniona uwanjani, kwa jinsi hali yangu ilivyo natumaini mchezo wa kwanza nitakuwa uwanjani,” alisema Fei Toto na kuongeza;

“Hizi ni mechi muhimu kwangu na timu kwa jumla, hivyo ni furaha yangu nikiona naendelea vyema kama inavyojulikana hakuna mchezaji anayetaka kukaa nje. Binafsi nimejipanga vilivyo natamani sana kuweka rekodi kimataifa kwa kushirikiana na kocha na wachezaji kwa jumla tuvuke makundi.”

FE 03


Hivi karibuni Mwanaspoti iliandika, Fei alishindwa kujiunga na Stars kutokana na tatizo la nyonga ambalo lilimpata katika mechi ya mwisho wa Ligi dhidi ya Namungo.

Azam imepangwa Kundi B la Kombe la Shirikisho Afrika sambamba na Wydad Casablanca ya Morocco, AS Maniema ya DR Congo na Nairobi United ya Kenya, huku mechi ya kwanza itakuwa ugenini  Novemba 23 kabla ya kurudi nyumbani wiki moja baadae kuisubiri Wydad.