JUZI Simba ilitoa ripoti ya kumkosa kipa namba moja, Moussa Camara, kwa kati ya wiki nane hadi 10 ikiwa siyo taarifa njema kwa mashabiki wa timu hiyo, licha ya uwepo wa kipa namba moja wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Yakoub Suleiman.
Kukosekana kwa Camara ni wazi kwamba kuna shida mahali, na huenda timu hiyo ikajikuta kwenye wakati mgumu mbele ya safari iwapo kipa huyo hatakuwa fiti ndani ya muda, huku kukiwa na wingi wa mechi inazokabiliwa nazo.
Simba inashiriki mashindano manne rasmi ikiwa ni Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho Bara, huku mengine yanayokuja ni Mapinduzi 2026 na Kombe la Muungano 2026.
Kutokana na hali inayopitia sasa timu hiyo kumkosa kipa wake namba moja, Camara, ni wazi kwamba wekundu hao wanaandamwa na ‘mzimu’ wa Aishi Manula, kipa aliyedumu muda mrefu kikosini hapo na kuondoka na rekodi kibao akiliweka jina lake miongoni mwa makipa bora Afrika.
Ipo hivi. Kwa miaka ya karibuni Simba imesajili makipa zaidi ya wanne tangu Manula achukue ufalme ndani ya kikosi hicho akijiunga na Simba kutokea Azam FC Agosti 2017.
Manula ndiye kipa pekee aliyehudumu muda mrefu ndani ya timu hiyo katika miaka ya hivi karibuni akiipa mafanikio katika michuano ya ndani na kimataifa, lakini wengine wote baada ya hapo hawajawa na misimu mingi licha ya kwamba aliondoka Simba msimu uliopita baada ya kumaliza mkataba wake.
Kabla ya Manula kusepa Simba, uongozi ulifanikiwa kunasa saini ya Ayoub Lakred aliyetua 2023/24 kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea FAR Rabat ya Morocco baada ya kuipa ubingwa wa Ligi Kuu timu hiyo.
Usajili wa Ayoub ulikuwa wa ghafla Simba kwani tayari ilikuwa imesajili kipa Mbrazili Jefferson Luiz ambaye aliishia Misri kwenye kambi ya maandalizi ya msimu huu (pre season) baada ya kupata majeraha.
Na kipa huyo licha ya kutoka kutwaa taji Morocco hakuanza msimu vizuri kutokana na uwepo wa Manula alianza kupata nafasi baada ya kuumia, huku ule msimu wa kwanza Ayoub akicheza mechi 14 za ligi kwa dakika 1260 na kuondoka na ‘clean sheets’ nane akiruhusu mabao 10. Lakred aliongeza mkataba uliomalizika msimu uliopita.
Itakumbukwa kwamba Lakred aliondoka Simba akiwa ameichezea kwa msimu mmoja mzima, lakini uliofuata hakuuanza wala kuumaliza akiwa golini kwani aliumia akiwa kambini Uturuki, ambako timu hiyo ilikuwa katika maandalizi ya msimu, suala ambalo liliulazimu uongozi wa Wekundu wa Msimbazi kumsajili Camara, ambaye kwa sasa ni majeruhi akiwa ndani ya msimu wake wa pili.
Manula aliumia Machi 22, 2024 akiwa anaitumikia timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) katika michuano maalumu ya Fifa Series iliyofanyika Baku, Azerbaijan.
Lakini, hata kabla ya michuano hiyo kipa huyo alikuwa ameingia kwenye sintofahamu na Simba, kwani katika mechi nyingi za mashindano ama hakuwepo kabisa benchini au alisugua huku Camara akicheza. Ikumbukwe kwamba wakati Manula akisugua pia Lakred alikuwa hajamaliza mkataba Msimbazi, ambapo golini asipodaka Camara alisimama Ally Salim kama msaidizi wake.
Katika mchezo dhidi ya Bulgaria uliochezwa Dalga Arena ambako Stars ilipoteza kwa bao 1-0, Manula alitoka uwanjani dakika ya 31 na nafasi yake ikachukuliwa na Kwesi Kawawa.
Lakred alikuwa miongoni mwa makipa waliotegemewa na Simba, lakini baada ya kucheza msimu mmoja na uongozi kumuongezea mkataba wa miaka miwili, matumaini hayo yalikatizwa baada ya kupata jeraha kubwa wakati wa maandalizi ya msimu 2024/25 nchini Misri.
Katika kipindi hicho, Simba ilikuwa kwenye harakati za kujiandaa kwa mashindano makubwa, jambo ambalo lilisababisha usajili wa Camara. Ujio wa Camara ndani ya Simba uliwasahaulisha mashabiki uwepo wa Lakred kutokana na ubora alioanza nao kipa huyo ambaye pia amecheza msimu mmoja uliopita akimaliza kinara Ligi Kuu Bara akiwa na ‘clean sheets’ 19 ukiwa ni msimu wake wa kwanza kati ya miwili Msimbazi.
Licha ya kuanza vizuri msimu akiwa na timu hiyo, kipa huyo ambaye alijimilikisha namba akimuondoa kabisa Manula Simba baada ya kumaliza mkataba kumalizika na kutimkia Azam FC, yeye pia ameumia na atakuwa nje kwa wiki kati ya nane hadi kumi huku ikielezwa mabosi wamerudi sokoni kusaka kipa mwingine mara tu dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa. Iwapo Camara ataondoka Simba ataacha swali moja; kuna nini? Kwani hakuna kipa baada ya zama za Manula atakayekuwa amedumu muda mrefu katika milingoti Msimbazi.
REKODI MANULA MATAJI (11)
Katika kipindi cha miaka mitano Manula ameiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara nne mfululizo (2017/18), (2018/19), (2019/20) na 2020/21.
Mbali na ligi ila amechukua pia mataji mawili mfululizo ya Kombe la Shirikisho la Azam maarufu (ASFC) msimu wa 2019/2020 na 2020/2021.
Kwenye Ngao ya Jamii amechukua mara nne mfululizo tangu 2017-2020 akiwa na kikosi hicho ambacho ndicho kinaongoza kutwaa taji hilo mara tisa (9) tangu lilipoanzishwa rasmi 2001, lingine likiwa ni la Mapinduzi alilotwaa mwaka huu (2022).
Manula (26) ndiye anayeongoza kwa kuweka rekodi ya kuchukua tuzo nyingi (5) za Ligi Kuu Bara kwenye nafasi anayocheza kwa kizazi cha sasa.
Manula alitwaa tuzo hizo misimu ya 2015/2016, 2016/2017 akiwa na Azam FC, huku akiwa na Simba ni 2017/2018, 2019/2020, 2020/21 kisha msimu wa 2021/22 alipinduliwa na Djigui Diarra wa Yanga ambaye nyavu zake hazikuguswa mara 15.
Endapo msimu wa 2018/19 ungekuwa na tuzo basi Manula angekuwa anamiliki sita, kwani aliiwezesha timu yake kunyakua ubingwa kwa kufikisha pointi 93 huku akifungwa mara 15.
Tangu kuwasili kwenye kikosi hicho, Manula amekutana na makipa wengi ila hadi sasa hakuna aliyeleta ushindani kwake wa kutishia nafasi yake hali inayomfanya kuendelea kutamba kila uchao. Miongoni mwa makipa hao ni Emmanuel Mseja, Said Mohamed ‘Nduda’, Deogratius Munish ‘Dida’, Jeremiah Kisubi, Ally Salim na Beno Kakolanya.