RAIS wa Yanga, Mhandisi Hersi Said amesema gharama za ada kwa Yanga Soccer School itategemea na maeneo ili kuhakikisha ndoto ya kila mtoto kuwa mchezaji inatimia.
Leo, Yanga imezindua Yanga Soccer School kwa lengo la kuendeleza vipaji vya watoto, ambapo mgeni rasmi katika shughuli hiyo alikuwa kocha wa zamani wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Pitso Mosimame.
Akizungumza na waandishi wa habari Upanga, Dar es Salaam, Hersi amesema gharama za ada kwa watoto hao zitaendana na maeneo akitolea mfano maeneo ya Muhimbili itakuwa ni Sh400,000 kwa mwezi, lakini sehemu zenye hali ya chini itapungu.
Ameongeza kuwa malengo ni kuhakikisha maeneo ya Dar wanapatikana watoto wengi na klabu kuwafikia waliopo mikoani.
“Tuna dhamira ya kuleta elimu ya mpira Tanzania ili kutoa fursa kwa vipaji vya watoto wadogo na tutachukua watoto kuanzia miaka 11, 14, 15. Tumeileta taaluma mapema na inajengwa kwenye misingi lengo ni kuandaa mpango endelevu,” amesema Hersi na kuongeza:
“Tumeanza na Dar kwa sasa, lakini hii itakwenda hadi mikoani kuna baadhi ya maeneo yatakuwa na gharama kubwa kulingana na maeneo, na maeneo mengine yatapunguzwa.”
Akimzungumzia Mosimane kwenye ushiriki mbalimbali wa matukio ya Yanga, Hersi amesema ni kocha mwenye uzoefu mkubwa Afrika, hivyo uwepo wake utaongeza kitu kwenye jambo hilo.”Mmoja wa makocha wenye mafaniko, mtu mwenye wasifu mkubwa alinihamasisha kufungua hiki kitu miaka mitatu iliyopita ana shule yake huko Afrika Kusini akiwa na wanafunzi zaidi ya 1000 na mmoja juzi alisajiliwa Mamelodi akitokea kwenye shule yake,” amesema Hersi.
“Kwenye mpira ametuzidi kila eneo na sisi tunahitaji kujifunza baadhi ya vitu na kutoa fursa kwa wenzetu.”
Kwa upande wake Pitso amesema ni wazo zuri waliloanzisha Yanga, kwani linaweza kusaidia kizazi cha Kitanzania kwa kuwa kikiwa na msingi wa soka kingali kidogo kitakuwa na mafanikio mazuri mbele ya safari.
“Yanga wanacheza kwa kushinda kwa sababu ni timu, lakini watoto wanahitaji kufundishwa mpira wa miguu, kudribo na huo ndio msingi wa shule,” amesema Mosimane.
“Nimewaona makocha ambao Yanga wamewateua, wanajua kufundisha soka la vijana, mazoezi gani lakini hata ushiriki wa wazazi naamini pamoja na vipaji itakuwa shule bora.”