MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara, JKT Queens wametupwa nje kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa mabao 4-1 na TP Mazembe.
Mtanange huo umepigwa kwenye Uwanja wa Suez Canal mjini Ismailia, Misri na kwenye kundi B JKT iliyomaliza nafasi ya tatu imeondolewa pamoja na Gaborone United iliyomaliza nafasi ya nne ikiambulia pointi moja.
Hii ni mara ya pili JKT inaondolewa hatua ya makundi kwenye michuano hiyo, kwani mara ya kwanza ilikuwa 2023 ilipomaliza nafasi ya tatu na pointi tatu.
Msimu huu mambo yalionekana kuwa magumu zaidi baada ya kupata sare mbili mfululizo ya kwanza dhidi ya Gaborone bila kufungana kisha ikatoka 1-1 na Asec Mimosas zilizoifabya kumaliza na pointi mbili.
Kwenye mechi hiyo JKT ilianza kwa kasi ikapata bao la mapema dakika ya 13 kupitia kwa Stumai Abdallah aliyemalizia faulo iliyochongwa na Anastazia Katunzi.
Dakika 12 baadaye Mazembe wakasawazisha kwa penalti kupitia Kasaj Yav dakika ya 25 na kufanya mzani kuwa sawa 1-1. Dakika nne baadaye mabingwa hao watetezi wa mashindano hayo wakaongeza la pili.
Mambo yalikuwa magumu zaidi baada ya JKT kuruhusu bao lingine la penalti na kuufanya mchezo utamatike kwa mavao 4-1 na Mazembe wakatinga nusu fainali ikiwa mara ya tatu kwao.