Kanisa Anglikana lawanoa walimu wa Sunday School

Kibaha. Kanisa Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam limeanza rasmi mafunzo kwa walimu wa Shule ya Jumapili (Sunday School) katika Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, yakilenga kuwaongezea uwezo wa ufundishaji wa masomo ya dini kwa kutumia mbinu za kisasa na zenye weledi zaidi.

Mafunzo hayo, yaliyofanyika leo Novemba 15, 2025 katika Achidikonari ya Kibaha, yanatolewa na wakufunzi kutoka Shirikisho la Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT) na yanahusisha zaidi ya walimu 30 kutoka makanisa mbalimbali ya eneo hilo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mchungaji Kiongozi wa Achidikonari ya Kibaha, Exavia Mpambichile amesema hatua hiyo ni muhimu kwa ajili ya kuboresha malezi ya kiroho kwa watoto ambao ndio msingi wa kanisa la sasa na la baadaye.

“Walimu wa Sunday School wanahitaji mbinu bora zinazomvutia mtoto wa kizazi cha sasa. Tunataka mtoto aweze kuelewa mafundisho ya Biblia kwa urahisi, kwa njia inayojenga imani na kumsaidia kukua katika maadili,” anasema Mchungaji Mpambichile.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo walimu katika kuandaa masomo yanayokidhi mahitaji ya makundi tofauti ya umri wa watoto, ili kuyafanya masomo yawe ya kuvutia, jumuishi na yenye matokeo chanya kwa watoto.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameelezea namna yalivyowaongezea uelewa na mbinu mpya za kufundisha.

Sara John, mmoja wa walimu, alisema mafunzo hayo yamemsaidia kupata mbinu bora za mawasiliano na namna ya kuwashirikisha watoto kikamilifu katika masomo ya dini.

Kwa upande wake, Msafiri Yohana amesema mafunzo hayo ni fursa adhimu kwa walimu wa Sunday School, kwani yanawajengea uwezo wa kuandaa masomo yanayomshawishi mtoto kujifunza kwa bidii na kuishi maisha yenye maadili na hofu ya Mungu.

“Lengo letu ni kujenga kizazi chenye uelewa wa kiimani unaolingana na changamoto za sasa, bila kupoteza misingi ya Biblia,” anasema.

Tangu kuingia kwake nchini mwaka 1864 kupitia wamisionari wa Church Missionary Society (CMS) kutoka Uingereza, Kanisa Anglikana limeendelea kuwa miongoni mwa taasisi zilizotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiroho. Wamisionari hao walijikita katika kuanzisha shule, vituo vya afya na huduma nyingine zilizosaidia jamii kwa miongo mingi.

Hadi sasa, Kanisa Anglikana linaendelea kuchangia katika sekta za elimu, afya, uongozi na malezi ya kiroho kupitia dayosisi zake nchini, huku likiimarisha programu za watoto, vijana na watu wazima kwa lengo la kuendeleza jamii yenye misingi imara ya kiimani na kimaadili.