CHAMA cha Soka Mkoa wa Ruvuma (FARU) kikishirikiana na wadau wa soka mkoani humo wapo katika hatua za mwisho kuifufua upya Majimaji Songea, ili kuhakikisha inarejea tena kwenye medani za soka.
Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Muungano na iliyowahi kutamba Ligi Kuu Bara, imepotea kwenye soka baada ya kufungiwa na kushushwa daraja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) msimu wa 2022/23 kutokana na kutofika uwanjani katika mechi zake za First League.
Hata hivyo, kabla ya kukutana na rungu hilo, chama hilo lilipitia magumu ikiwamo kukwama hotelini jijini Dar es Salaam kwa kushindwa kulipa gharama za malazi kabla ya wadau wa soka akiwamo staa wa zamani wa Simba, Erasto Nyoni kuokoa jahazi.
Kama haitoshi, tangu Majimaji ipotee katika ramani za soka, Ruvuma haijawa na burudani kali licha ya uwapo wa Songea United na Tunduru Korosho ambazo hazijafanya vizuri kufikia rekodi na historia ya ‘Wanalizombe’.
Mwenyekiti wa DARU, Kamwanga Tambwe ameliambia Mwanaspoti, hadi sasa tayari faini iliyopigwa na timu hiyo wameilipa huku mchakato wa kuirejesha ukiendelea.
Tambwe amesema wakati ikirudi timu hiyo kongwe haitakuwa katika mfumo uleule wa wanachama badala yake itakuwa katika muonekano mpya wa kampuni baada ya wadau kuamua kuwekeza nguvu huko.
“Faini imelipwa na adhabu ya muda iliyofungiwa imepita, hivyo itashiriki ligi ya Mkoa inayotarajia kuanza mapema mwezi ujao Desemba, kimsingi haitakuwa tena kwenye mfumo wa wanachama,” amesema Tambwe na kuongeza;
“Wapo wadau ambao tunashirikiana nao na sisi FARU (Chama cha Soka) ndio wasimamizi wa mchakato huu, matarajio yetu ni aidha kununua timu ya daraja la juu na kuibadili jina au kuendelea na Majimaji yenyewe.”
Kigogo huyo amesema, kiu ya wadau na mashabiki wa soka mkoani humo ni kuona Majimaji ‘Wanalizombe’ ikirudi kwenye anga zake kutokana na mapenzi waliyonayo kwa muda mrefu.