KOCHA Mkuu wa Mashujaa, Salum Mayanga amesema kikosi kinaendelea kuimarika na kutengeneza muunganiko ili kutoa ushindani kwenye Ligi Kuu Bara aliyodai kuwa ni ngumu na bora tofauti na misimu ya nyuma.
Kikosi cha timu hiyo Jumatatu kilirudi kwenye uwanja wa mazoezi kwa ajili ya kujiweka sawa na mchezo wa ligi dhidi ya Mbeya City utakaopigwa Novemba 22.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mayanga amesema maandalizi yanakwenda vizuri na kikosi chake kipo kwenye hali nzuri ya ushindani na anaamini wanatambua umuhimu wa mchezo ulio mbele yao.
“Tuna mechi ngumu dhidi ya Mbeya City ni timu ambayo imerudi vizuri ikifanya usajili mzuri ili kuwa bora tunatakiwa kujiandaa vizuri na ndicho kinachofanyika matarajio yetu ni kupata matokeo licha ya kwamba haitakuwa rahisi,” amesema Mayanga aliyewahi kuinoa Mbeya City kabla ya kutua Mashujaa aliyeongeza:
“Tutakuwa nyumbani tena na mechi ya mwisho kwenye uwanja wetu tumepata matokeo mazuri dhidi ya Namungo kwa ushindi wa bao 1-0 tunahitaji kuwa na mwendelezo huo mchezo ujao ili kujiwekea mazingira mazuri kwenye msimamo.”
Mayanga amesema sasa anafanyia kazi kujenga utimamu wa mwili kwa wachezaji wake baada ya kutoka mapumziko na baada ya hapo atafanya kazi ya kusawazisha makosa aliyoyaona akiitaja safu ya ushambuliaji na ulinzi kuwa kuna mapungufu.
“Mapungufu hayawezi kukosekana muhimu ni utimamu wa mwili mzuri vitu vingine vinaelezeka na nimekuwa nikifanyia kazi kila mchezo nafikiri mazuri yanaonekana na mapungufu pia yanafanyiwa kazi.”
Mashujaa kwa sasa ipo katika nafasi ya tano ikiwa na pointi nane kutokana na mechi sita, ikishinda mbili kutoka sare mbili na kupoteza mbili huku ikifunga mabao manne na kufungwa manne.