Shinyanga. Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amewahimiza wananchi wa wilaya ya Shinyanga hususani watumishi wa umma kujenga tabia ya kupima afya mara kwani kutokufanya hivyo kunasababisha magonjwa ambavyo yangeweza kutibika mapema kuchukua muda mrefu na gharama.
Akizungumza leo Novemba 15, 2025 katika kikao cha uwasilishaji taarifa ya lishe kwa Manispaa ya Shinyanga, kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa mkoani Shinyanga, Mtatiro ameeleza kuwa ni vyema jamii ikabadilika na kujenga tabia ya kufanya vipimo mara kwa mara,
“Watumishi wa Umma jengeni tabia ya kupima afya, ni mhimu zaidi tukajenga tabia ya kufanya vipimo vya afya zetu mara kwa mara sio hadi uugue ndipo uende hospitali kwa ajili ya matibabu, watumishi wa Umma tuwe mfano wa kuigwa kwa wananchi tujali afya zetu kwani ndiyo kila kitu,,” amesema Wakili Mtatiro.
Pia ameongeza kuwa, “Wakina mama mnatakiwa kupima saratani ya shingo ya kizazi angalau mara moja kwa kila miaka miwili ugonjwa huu umekuwa ni tatizo na mengi pia yamekuwa yakisababishwa na msongo wa mawazo ni vyema jamii ikabadilika,” amesema Mtatiro.
Kwa upande mwingine Mtatiro amewataka wataalamu wa afya kutoa elimu ya mara kwa mara kwa watumishi pamoja na wananchi wote ili wachukue tahadhali mapema ya magonjwa hatari katika jamii pamoja na kusisitiza juu ya masuala ya lishe bora katika jamii.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa lishe kwa Manispaa ya Shinyanga kwa niaba ya mratibu wa lishe Misango George amesema katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2025, jumla ya watoto 135 walibainika kuwa na utapiamlo, kwa walioandikishwa kwenye matibabu,
“Kati ya watoto walioandikishwa watoto 135 waligundulika kuwa na utapiamlo na watoto 122 wamepona na waliobaki wanaendelea na matibabu katika hospitali na vituo vya afya katika Manispaa ya Shinyanga” amesema George.
Wakichangia taarifa hiyo wajumbe wameshauri kuendelea na mikakati ya kuhamasisha shughuli za lishe shuleni na kwenye jamii ili kufikia lengo la mkataba wa lishe.