Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba leo Novemba 15, 2025, amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kutoa maagizo mazito kwa Wizara ya Afya, Bohari ya Dawa (MSD) na hospitali zote nchini kuhusu mwelekeo mpya wa utoaji huduma bora za afya, hususan kwa wajawazito na upatikanaji wa dawa.
Akizungumza katika ya hospitali hiyo, Dk Mwigulu amesisitiza kuwa wajawazito wanapaswa kupatiwa huduma mara moja kwa kuwa kuchelewa kwao kunaweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto.
“Hakuna mama mjamzito anayepaswa kusubiri foleni ya mapokezi. Wafikapo hospitalini wahudumiwe haraka ili kuokoa maisha,” ameagiza.
Katika maelekezo yake kwa Wizara ya Afya na MSD, Dk Mwigulu ameitaka watendaji wa serikali kuhakikisha upatikanaji wa uhakika dawa katika hospitali zote, ikizingatia mahitaji ya maeneo husika.
Amesema haipendezi kwa wananchi kufanyiwa vipimo hospitalini kisha kuambiwa wanunue dawa nje.
“Kama duka binafsi linaweza kupata dawa, inawezekanaje hospitali za Serikali zikose? Naagiza hospitali zote ziwe na dawa,” amesisitiza.
Aidha, Waziri Mkuu amezielekeza hospitali kuhakikisha kunakuwepo vifaa vya usafi binafsi vya dharura katika wodi za wazazi, ikiwemo beseni na ndoo kwa ajili ya mama wajawazito wasiokuwa na uwezo wa kuvipata mara moja wanapofika.
“Ujauzito si tukio la kushtukiza. Lazima tuwe na vifaa hivi muda wote, hasa katika hospitali za Serikali.”
Dk Mwigulu ametumia ziara hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kuboresha huduma za afya nchini, zikiwemo dawa, vifaa tiba na miundombinu ya hospitali. Wananchi waliokutana naye hospitalini walimueleza kuwa huduma zimeimarika na wanahudumiwa kwa uangalifu wa karibu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameonya hospitali zinazopokea malipo kwa njia zisizo rasmi na kuagiza zizingatie mifumo sahihi ya malipo ya serikali ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo.
Amesema baadhi ya hospitali hupokea malipo kwa njia tofauti, jambo linalokiuka taratibu na kuathiri ufanisi wa huduma.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Dodoma Dk Ernest Ibenzi amesema katika hospitali hiyo hawana shida na watumishi kwani wakati wote wanatambua wajibu wao na kiwapasacho kufanya.
Dk Ibenzi amesema upo uwekezaji mkubwa wa huduma za afya ndiyo maana kila mmoja anatimiza wajibu wake akitaja namna wagonjwa walivyosifia huduma za hapo mbele ya Waziri Mkuu ambaye hawakujua kama angetembelea eneo hilo.
Mmoja wa ndugu waliokuwa na wagonjwa hapo Ester Lukasi ameeleza namna huduma za Hospitali hiyo kwa sasa zilivyo rafiki kwa wagonjwa hasa wajawazito tofauti na miaka ya nyuma.
Ester amesema licha ya kutokupata huduma kwa asilimia miamoja, lakini wahudumu wa hapo wamekuwa wepesi katika kuwatembelea wagonjwa na kushauri nini kifanyike lakini kwa huduma ya watoto amesema madaktari wako makini sana.