Dar es Salaam. Shura ya Maimamu Tanzania imetoa msimamo wake kuhusu mustakabali wa maridhiano ya kitaifa kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, ikisisitiza kuwa jitihada za kujenga umoja wa kitaifa zinapaswa kuzingatia ukweli, uadilifu na uwajibikaji wa mamlaka zote zilizohusika katika mchakato wa uchaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi, Novemba 16, 2025 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Shura hiyo, Sheikh Issa Ponda amesema kikao cha taasisi hiyo kimechambua kwa kina mwenendo wa uchaguzi huo na kutoa mapendekezo ya namna ya kufanikisha maridhiano yatakayorejesha utulivu na mshikamano nchini.
Katika maelezo yake ya utangulizi, Sheikh Ponda amekumbusha nafasi ya Shura ya Maimamu katika jamii, akieleza kuwa kwa miaka mingi taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza maadili ya kijamii na kisiasa, kushiriki uangalizi wa chaguzi na kutoa ushauri kwa maslahi mapana ya taifa.
Amesema hatua yao ya kutoa msimamo ni sehemu ya wajibu wao wa kijamii na kidini katika kulinda haki, amani na utu.
Sheikh Ponda amesema utafiti wao umebaini kuwa mchakato wa uchaguzi, kuanzia uandikishaji wa wapiga kura, upigaji kura hadi kutangazwa kwa matokeo, ulikumbwa na dosari zilizojitokeza wazi.
Kwa mujibu wake, changamoto hizo zinaonesha hitaji la mabadiliko ya dharura katika mifumo ya uchaguzi na uwajibikaji wa taasisi za dola.
Ameongeza kuwa kasoro hizo zimeathiri sura ya uchaguzi na kupunguza imani ya wananchi katika mchakato huo, ikiwamo kutokea kwa vurugu katika baadhi ya maeneo na taarifa za vifo vya raia vilivyotokana na vurugu hizo na wengine kujeruhiwa na kutojulikana walipo.
“Tunalaani mauaji hayo. Tunatoa salamu za rambirambi kwa familia zote zilizoondokewa na wapendwa wao, tukitumaini kuwa amani itarejea nchini,” amesema.
Hata hivyo, jana Ijumaa Novemba 14, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizindua Bunge la 13 jijini Dodoma, aliahidi kuunda Tume maalumu ya maridhiano kwa lengo la kumaliza mzozo uliotokea na kuliunganisha taifa.
Katika hotuba yake, Rais Samia alilaani mauaji, akatangaza msamaha kwa watuhumiwa ambao wanashikiliwa huku akimuagiza waliokumbwa na machafuko hayo na kutoa wito kwa wadau pamoja na vijana kudumisha amani ili kuwezesha maridhiano ya kitaifa.
Hata hivyo, Shura ya Maimamu imesisitiza kuwa hatua yoyote ya maridhiano haitakuwa na maana iwapo haitashughulikia chanzo cha migogoro na madhara yaliyotokea.
Sheikh Ponda amesema misingi ya haki na uadilifu ndiyo nguzo kuu ya kujenga jamii imara na yenye mshikamano.
Akitoa mapendekezo ya taasisi hiyo, Sheikh Ponda amesema maridhiano ya kitaifa yanapaswa kupewa kipaumbele kuliko matamko ya kisiasa.
“Maridhiano yanaweza kufanikiwa endapo yatakuwa ya dhati, yasiyoegemea upande wowote na yatakayoshirikisha wadau wote muhimu,” amesema.
Kuhusu Tume ya maridhiano iliyopendekezwa na Rais Samia, Shura ya Maimamu imeshauri kuwa ipo haja ya kuelewa kwa kina uhalisia wa yaliyotokea na kushughulikia mizizi ya migogoro badala ya kuunda tume inayotokana na mamlaka zinazolalamikiwa.
Imeeleza kuwa maridhiano hayo yanapaswa kuongozwa na mtu mwenye heshima, uzoefu na anayekubalika na pande zote, kama kiongozi mstaafu, kiongozi wa dini au mwakilishi wa taasisi ya haki za binadamu.
Pia, Shura hiyo imewataka viongozi wastaafu, vyama vya siasa, taasisi za haki za binadamu na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika mchakato huo ili kuhakikisha maridhiano yanakuwa ya kweli na yenye tija kwa taifa.
Katika mapendekezo mengine, Shura ya Maimamu imesisitiza umuhimu wa kuharakisha mchakato wa Katiba mpya, ikieleza kuwa Katiba mpya ni sehemu muhimu ya kuondoa chanzo cha migogoro ya kisiasa na kuimarisha uwajibikaji wa taasisi za kiserikali na uchaguzi. “Tunaiomba serikali kuanza mara moja mchakato wa Katiba mpya ili Watanzania waandike Katiba wanayoitaka,” amesema Sheikh Ponda.
Katika hotuba yake ya jana, Rais Samia aliahidi kuanzisha mchakato wa Katiba mpya ndani ya siku 100 za mwanzo madarakani, akibainisha kuwa maridhiano ni hatua ya msingi kabla ya kuanza safari hiyo.
Kwa ujumla, Shura ya Maimamu imesisitiza kuwa mustakabali wa amani na umoja nchini unategemea hatua thabiti na za wazi zinazojali utu, haki na ukweli. Imeeleza kuwa msimamo wake unalenga kuhimiza majadiliano yenye tija, kuondoa wasiwasi wa wananchi na kujenga upya mahusiano kati ya raia, vyama vya siasa na taasisi za dola.