SMG ataja hekima, ugumu soka la wanawake

KOCHA msaidizi wa Yanga Princess, Said Maulid ‘SMG’ amesema amepata uzoefu tofauti kuwafundisha timu za wanawake, lakini kitu kikubwa ili kufanikiwa hasira ni lazima ziwe mbali.

Aliifafanua kauli yake namna wachezaji wa kike wanavyokuwa na ‘mudi’ tofauti, jambo ambalo linachangia upokeaji wa maelekezo ya makocha kuchukua muda mrefu tofauti na wanaume.

“Soka la wanawake ni gumu kuliko la wanaume. Kusema ukweli nasaidiwa sana namna ya kuendana nao na kocha mkuu Edina Lema, lakini wamenipa uzoefu mkubwa wa kujua namna ya kutumia hekima ili kuendana nao,” amesema SMG na kuongeza:

“Kila mtu ana mudi zake leo anaweza akaamka vizuri kesho akawa mtu tofauti kabisa, sasa kocha akiwa na hasira hawezi kumudu kuendana nao lazima ufanye kazi zaidi ya ualimu uliosomea.”

SM 01


SMG aliye na Diploma A ya CAF amesema mbali na soka la wanawake anajivunia kuona vijana aliowanoa Yanga B wanafanya vizuri katika timu walizopo na  baadhi yao ni Omary Chibada (Mbeya City), Ismail Mpank ukiacha Clement Mzize anayeitumikia Yanga na anafanya kazi nzuri.

Kuhusiana na kuendelea kufanya kazi ya takwimu za wachezaji, mkongwe huyo amesema: “Nilisoma kozi hiyo wakati nipo Angola ambako niliichezea timu hiyo Onze Bravos na bado nikafanya kazi ya kukusanya data za wachezaji na kumpelekea kocha baada ya kustaafu  uwanjani.”