Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeanzisha kampeni ya kutoa elimu ya usafiri salama wa majini katika Wilaya ya Chato mkoani Geita eneo ambalo limeendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa kutokuripoti ajali za majini kwa muda mrefu.
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu ya usafiri salama wa majini kwa Wavuvi wa Wilaya hiyo Afisa Mfawidhi wa TASAC mkoa wa Geita, Bw. Godfrey Chegere, amesema elimu hiyo inalenga kuwasaidia wavuvi kutii sheria bila shuruti, kuboresha usalama, na kujilinda wanapokuwa majini.
Amesema tangu Januari 2024 hakuna ajali yoyote iliyoripotiwa Chato kutokana na utii wa sheria na mwitikio mzuri wa wavuvi.
Kwa upande wake, Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Chato, Bi. Avodia Sylivester, amesema ushirikiano kati yao na TASAC umepunguza ajali zilizokuwa zikisababisha vifo 20–30 kwa mwaka, kupitia elimu ya utabiri wa hali ya hewa, matumizi ya life jacket na ubora wa vyombo.
Wavuvi nao wamepongeza juhudi hizo wakisema elimu imesaidia kuepusha ajali na kuongeza usalama.
Wanjala Sonde, mvuvi wa Chato Beach, alisema:
“Tangu elimu ianze kutolewa, hatujapata ajali hata moja. Tunashukuru TASAC.”
Kwa upande wake, Christopher Chrizostom, abiria wa mwalo wa Kasenda, ameomba mifumo ya kudhibiti wanaokaidi kuvaa life jacket kuimarishwa zaidi.
TASAC imeahidi kuendelea na kampeni hii nchi nzima ili kuhakikisha usafiri wa majini unakuwa salama, wenye ubora na unaozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.


