Rais Samia Suluhu Hassan amelifungua rasmi bunge la 13 Jijini Dodoma na moja kati ya mambo ambayo yamenigusa kama raia mwema, ni kauli inayoashiria kukiri kuna mahali tumeteleza na akanyoosha mkono wa kutamani maridhiano ya kitaifa.
Tukae kama watanzania kwa njia za amani, wananchi waweke hasira kando na mihemko, serikali iweke mbele dhamira iliyotajwa kwenye ibara ya 8(1)(a), (b) na (c) ya Katiba, serikali ikae na wananchi kwa kuwa wao ndio wanaotoa mamlaka.
Tuharakishe mazungumzo haya ya maridhiano tukitambua tuna deal (kushughulika) na kizazi “complex” (tata sana) hivyo tusishupaze shingo, tujishushe chini kwa maslahi mapana ya taifa letu na machawa tuwaweke pembeni kwani ni sehemu ya waliotufikisha hapa tulipo sasa.
Wala tusijidanganye kuwa adui wa kisiasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa bado kwa sehemu kubwa ni Chadema, la hasha, kwa tulichokiona Oktoba 29 ni lazima tukiri kuwa waliokuwa kinyume na Serikali ya CCM ni wananchi.
Lazima niseme mapema kabisa, kwamba pamoja na dhamira njema ya Rais Samia, ni lazima kila upande ujishushe na kukubali kupoteza walau asilimia 10-40 ya msimamo wake, lakini kila upande ukijiona ni bora kuliko mwingine, hatutoboi.
Sitamani na naamini wengi hawatamani kile kilichotokea siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025 na siku tano zilizofuata kijirudie tena, kwa sababu hatutaki tena kuzika wapendwa wetu na tusema “never and never again”, kisijirudie tena.
Nimelipa suala la uhai umuhimu mkubwa si kwa sababu sitambui wapo waliojeruhiwa au mali zao kuibwa, kuchomwa au kuharibiwa, la hasha bali ni kwa sababu unalindwa kikatiba chini ya ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzania ya 1977.
Ninaamini mamlaka zitatoa idadi halisi ya waliuawa badala ya kuwaacha watanzania kuegemea takwimu za vyombo vya Habari vya kimataifa ambazo kwa kweli zinatisha kuzisikia na ndizo zimeongeza hasira na chuki dhidi ya Serikali.
Kabla ya kujadili kwa undani maridhiano, ni muhimu nikaweka wazi msimamo wangu kuwa tulichokishuhudia Oktoba 29,2025 hayakuwa maandamano ya amani, kwani yalikosa sifa na vigezo vyote vya maandamano ya amani.
Iwe ni maandamano ya amani au sio ya amani, ni muhimu sana kujua ni wakati gani maandamano yanakuwa halali kisheria na ni wakati gani maandamano yanakuwa haramu na kusababisha mvutano na vyombo vya Dola.
Bila kufahamu hili, tunaweza kujikuta tunaiingiza nchi na watanzania katika machafuko hata kama wanaotaka kuandamana wana hoja kiasi gani, kwa sababu jambo lolote linalofanyika nje ya sheria linakosa uhalali wa kisheria.
Kwa Tanzania, Ibara ya 20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 ambayo ni sheria mama, inayosema kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani.
Inatoa ruksa kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au mengine.
Tanzania pia imeridhia mkataba unaojulikana kama African Charter of Human and Peoples Rights wa 1981 ambao unasema kila mtu anayo haki kukusanyika na watu wengine, lakini inaweza kuzuiwa na sheria kwa sababu za usalama wa taifa.
Kwa Tanzania, sheria inataka waandaaji wa maandamano ya amani, wanatakiwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi saa 48 kabla ya muda waliopanga kuandamana, na Polisi wana mamlaka ya kuyaruhusu au kuyazuia kwa sababu za kiusalama.
Ukisoma kifungu cha 11(4) cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019 kinasema pale ambapo maandamano yanaandaliwa na chama cha siasa, basi ni lazima waijulishe polisi saa 48 kabla ya maandamano ili watoe ulinzi.
Kifungu kidogo cha (5) kinasema taarifa ya kwenda polisi ni lazima ionyeshe muda na mahali maandamano yatafanyika na agenda na baada ya kutoa taarifa wanaweza kuendelea, isipokuwa kama watapata zuio la polisi.
Sasa tuje kwenye hicho kinachoitwa maandamano ya Oktoba 29, 2025, yameandaliwa na nani, taarifa imetolewa kwa mkuu gani wa kituo cha Polisi (OCS), nini agenda ya maandamano na je, Polisi waliyapa baraka?
Ukiyafuatilia, utagundua hakuna taasisi au kundi rasmi kwa hapa nchini ambao wameyaandaa wala hakuna chama cha siasa kimeyaandaa, bali yameandaliwa na watu walio nje ya nchi kupitia mitandao ya kijamii.
Nakubali, maandamano ya amani ni njia mojawapo ya kufikisha ujumbe kuwa kundi fulani halikubaliani na jambo fulani, lakini unafanyaje maandamano ya amani hayana kibali cha Polisi wakati unajua fika hilo ni takwa la kisheria?
Ninaposema hivi, nisichukuliwe kama nahalalisha mauaji yale yaliyofanyika, iwe kwa walioandamana, waliopora mali au waliouawa hata hawapo kwenye maandamano. Ninaamini Tume hii ya Rais itatuambia kama ilikuwa halali.
Tunapotafakari suala hili la maridhiano ni muhimu sana tukafahamu nini hasa wanachokitaka katika maridhiano hayo ili kuliweka taifa letu salama, lakini tukishajua matakwa yao, tujue kuna kanuni 8 zinazosimamia maridhiano ya kweli.
Mbali na kutoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwaombea majeruhi wapone haraka, Rais ameenda mbali na kusema Serikali itaunda Tume ya kuchunguza yaliyotokea (Enquiry commission) ili kujua kiini cha tatizo.
Naomba ninukuu maneno muhimu sana ya Rais kwamba “Kama Taifa tunaendelea kujifunza na kujirekebisha. Tuendelee kujifunza, tujirekebishe na kukubaliana jinsi ya kuiendesha nchi yetu kidemokrasia kwa kuzingatia mil ana desturi zetu”
Taarifa ya Tume hiyo ambayo Rais anaiunda kupitia kifungu cha 3(1) cha sheria ya Tume ya Uchunguzi sura ya 32, naamini itakuwa huru na haitahusisha makundi yale ya taasisi ama watu ambao wanatajwa kwa majina kutufikisha hapa tulipo.
Kabla ya kuzisema kanuni 8 za maridhiano nilizotangulia kuzisema, ni muhimu nikasema walau kwa kifupi, nini kinasemwa na vijana huku mtaani kuwa ndio kiliwasukuma kuandamana Oktoba 29 na kuna vuguvugu la kurudia Desemba 9.
Wanachokitaka kiwepo mezani katika majadiliano ya maridhiano ni kuona maridhiano yasiwe ni ya wanasiasa pekee, idadi ya waliuawa na kujeruhiwa itajwe na serikali iseme imechukua hatua gani kwa waliofanya mauaji yale ya kutisha.
Ikumbukwe wapo waliouawa ambao walikuwa majumbani mwao au katika mazingira ambayo hayakuwa ya vurugu tena watoto wadogo kabisa wengine chini ya umri wa miaka miwili na kwa hakika wanastahili fidia.
Kilio kikubwa ambacho wala si kigeni kwani kilianza hata kabla ya nchi yetu kuingia katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1977 ni kuandikwa kwa Katiba mpya iliyobeba maoni ya wananchi, ambayo itazaa kiuhalisia, Tume Huru ya Uchaguzi.
Lakini madai mengine ni kutaka kukomeshwa kwa utekaji, kupotezwa kwa watu (enforced disappearance) na mauaji yanayodaiwa kufanywa na vyombo vya Dola (extra judicial killing) na watu wote waliotekwa na kupotezwa warejeshwe.
Mbali na madai hayo, wanataka Jeshi la Polisi lifumuliwe na kusukwa upya, ukamataji holela unaofanywa na Polisi na vyombo vingine ukomeshwe, mahojiano yanayoambatana na mateso yakomeshwe na kila kitu kiwe ndani ya sheria.
Mambo mengine ni ya jumla kwamba wanahitaji uwepo wa taasisi imara (strong institutions) kama Mahakama, Bunge na Jeshi la Polisi ambazo ni huru katika utendaji wake na maamuzi yake yasionekane yanaegemea upande mmoja.
Sasa tunakwenda kwenye mazungumzo ya maridhiano, nini kitatuongoza?
Kanuni zinataka pia kuwepo kukiri makosa yaliyotendeka, kuheshimu utu wa kila anayeshiriki maridhiano, kusikiliza upande wa pili, kuomba radhi na kuwajibika, kuchukua hatua Madhubuti kuponya maumivu na kujenga kuaminiana.
Lakini kanuni hizo pia zinataka kuwepo na ustahimilivu na kulenga kuponya badala tu ya kwamba umewapa nafasi sawa ya kusema na mwisho ni lazima kuwe na uwajibikaji na kuendelea na mazungumzo hata nyakati ziwe ngumu kiasi gani.
Hizo kanuni zinatumika katika maridhiano kwenye jamii lakini kuna kanuni ambazo zinasimamia maridhiano ya kisiasa ambazo nazo ni muhimu sana kuzifahamu.
Kanuni ya kwanza inataka wahusika wakiri kuna jambo limetendeka kabla ya kukaa mezani ambalo limeumiza na linahitaji kutafutiwa dawa, na kanuni ya pili inataka kuwapo majadiliano shirikishi yakisimamia na msuluhishi huru anayekubalika.
Tatu kanuni inataka kuwepo kwa utawala wa sheria, kwamba kuwepo na mchakato wa kisheria utakaowawajibisha waliotenda matendo hayo mabaya lakini pia kutoa msamahaka (amnesty) kwa wahusika wanaokiri na kujitia walichofanya.
Kanuni ya nne ni kama moja ya zile 4R za mama Samia kwani inataka kuwapo kwa mabadiliko (reforms) ya kitaasisi na kuzifanyia mapinduzi makubwa taasisi kama Polisi, Mahakama na mfumo mzima wa utumishi wa umma Tanzania.
Kwa upande wake, kanuni ya tano inataka kugawa upya rasilimali, kutoa fidia, au kuunda nafasi za kazi ili kuziba pengo la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, ambalo lililoundwa na dhuluma za zamani ambazo zikalifikisha taifa hapo lilipofika.
Sita ni lazima umoja wa kitaifa uonekane kwa vitendo na si matabaka, kanuni ya saba inataka kuwepo kwa chombo huru ambacho kitawajibika kufuatilia maendeleo ya maridhiano na kila kitu kifanyike kwa uwazi na ukweli.
Hizo ndio kanuni za maridhiano, lakini kila mmoja akienda katika maridhiano huku umeficha mapanga nyuma, hayo maridhiano hayafiki mbali. Tutarudi kule kule tulipokwama kwenye zile 4R za Rais Samia. Amini nawaambia.