Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kueleza dhamira ya kuendeleza mchakato wa maridhiano, wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, wachambuzi wa masuala ya siasa, vyama vya siasa na asasi za kiraia, wamebainisha namna bora ya kufanikisha safari hiyo ili kufikia mustakabali mwema wa Taifa.
Wengi wao wamesisitiza umuhimu wa maridhiano jumuishi yatakayozingatia ukweli, haki, uadilifu, uzalendo na thamani ya amani, huku baadhi wakitaka uchunguzi wa kina kufanywa kuhusu matukio ya vurugu za Oktoba 29.
Akizindua Bunge la 13 jijini Dodoma jana Ijumaa Novemba 14, 2025, Rais Samia alisema dhamira yake ya kuhimiza maridhiano katika muhula wake wa kwanza ilikwamishwa na baadhi ya wadau, lakini katika awamu hii hatakata tamaa katika kuurejesha mkono wa maelewano.
Alifafanua kuwa wakati wa muhula wa kwanza alianzisha falsafa ya 4R kwa lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa na kwamba, Serikali imeendelea kuonyesha utayari wa kujenga misingi ya maridhiano kwa manufaa ya Taifa.
“Kwa kuwa Watanzania wamenipa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi hii, sitachoka kunyoosha tena mkono wa maridhiano. Ni matumaini yangu kuwa wadau wa kisiasa wataupokea kwa dhati mkono wa maelewano ili kwa pamoja tujenge mazingira bora kwa Taifa letu,” alisema Rais Samia.
Akizungumzia kauli hiyo leo Jumamosi Novemba 15, 2025, mchambuzi wa siasa, Ali Makame amesema maridhiano ni hatua muhimu endapo wadau wataweka mbele uzalendo na kutanguliza amani badala ya ushabiki wa kisiasa.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa Serikali inapaswa kuondoa mtazamo wa kuwadhania wapinzani kama watu wasiostahili kusikilizwa, akibainisha kuwa dhana hiyo inaweza kuathiri nguvu ya maridhiano yenye lengo la kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Mchambuzi mwingine, Nassor Seif Amour, ametaja umuhimu wa viongozi wa kisiasa na dini kukaa pamoja na Serikali ili kupata mwafaka wa kweli.
“Ukiachia vyama vya siasa pekee vina mitazamo yao na huenda vikaweka masharti yao. Lakini viongozi wa dini hawapo ndani ya siasa na wanaweza kusaidia kupata sura ya pamoja,” amesema mchambuzi huyo na kuongeza kuwa maafa yaliyoshuhudiwa hayakuwa ya kisiasa pekee, bali ya kibinadamu, hivyo inafaa makundi hayo mawili kushirikishwa ili kupata mwafaka mpana.
Amour amesema maridhiano ya kweli yanahitaji pande zinazokutana kukubali kuwa si kila wanachokitaka watakipata, kwa sababu mchakato huo ni wa kutoa na kupokea. Amehimiza kushirikishwa kwa makundi tofauti ikiwamo wataalamu wa uchumi ili kupata uelewa mpana wa changamoto zilizopo.
Kwa upande wake, Keneth Nashon amesisitiza kuwa maridhiano yanayohitajika ni yale yatakayothamini uhuru wa kujieleza na kuondoa dhana ya kuwajibishana kwa misingi ya hisia za kisiasa.
Amebainisha kuwa mchakato wa uchaguzi uliopita haukuwa sawa kwa sababu baadhi ya vyama havikupata fursa ya kushiriki kikamilifu, licha ya kuwasilisha maombi ya kubadilisha mfumo wa uchaguzi.
Mchambuzi wa siasa na jamii, Kiama Mwaimu amesema maridhiano yanatakiwa kuwa ya kitaasisi na jumuishi, yakihusisha asasi mbalimbali na watu mashuhuri.
“Watu hawa wakikaa na kujadili kwa pamoja, maoni yao yanaweza kuongezewa nguvu na yale ya wanasiasa na Serikali,” amesema.
Kwa upande wake Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Dk Ananilea Nkya amesema yeye haoni uwezekano wa maridhiano kufanikiwa bila vijana na wananchi kusikilizwa madai yao.
Dk Nkya amesema maridhiano hayawezi kuleta suluhu iwapo wahusika wakuu wenye hoja na maumivu hawapati nafasi ya kujieleza.
“Hayo maridhiano yatakuwa kati ya nani na nani wakati vijana na wananchi wanaobeba hoja hawasikilizwi?” amehoji.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa George Kahangwa, amependekeza kuundwa kwa tume ya kijaji au Baraza la Maridhiano la Taifa litakalojumuisha watu wanaoaminika na kuheshimika katika jamii.
Ameeleza maridhiano ya kweli hayawezi kupatikana bila kushughulikia tofauti za kijamii na kisiasa zilizojitokeza katika miaka ya karibuni.
Mchambuzi wa siasa na diplomasia, Deus Kibamba amesema mchakato wa maridhiano umeathiriwa na mauaji na matukio ya kupotea kwa watu katika kipindi cha uchaguzi.
Amesema hali hiyo inaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa mustakabali wa maridhiano endapo haitashughulikiwa kwanza kwa uaminifu.
Amependekeza uchunguzi huru wa kimataifa ufanyike ili ukweli wote ujulikane na wale waliofungwa au kuhusishwa na kesi zinazodaiwa kutungwa waachiwe huru mara moja.
Amesema ni baada ya ukweli kujulikana ndipo Watanzania wanaweza kuombana radhi, kusameheana na kujadiliana kwa nia njema juu ya mustakabali wa Taifa.
Kwa maoni yake, “dawa” ya kudumu ya kukomesha migogoro ya kisiasa ni kuandikwa kwa Katiba mpya isiyohodhiwa na masilahi ya wanasiasa.
TEC yataka uchunguzi kwanza
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa tamko likikemea vikali vurugu za Oktoba 29, 2025 na kutaka uchunguzi huru ufanyike kwanza kabla ya maridhiano.
Limesema uchunguzi huo ushirikishe wadau wa ndani na nje ya nchi huku likisisitiza kuwa watu wote waliokamatwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi waachiwe huru, sambamba na kukumbusha umuhimu wa kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya.
Pia, TEC imetoa wito kwa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wawajibike au kuwajibishwa na mamlaka zao za uteuzi kutokana na kadhia hiyo iliyotokea.
Akisoma tafakuri ya pamoja ya maaskofu, iliyotokana na sala na maombi yaliyofanyika kwa siku nne kuanzia Novemba 11 hadi 14, Rais wa TEC, Askofu Wolfgang Pisa amesema kanisa limesikitishwa na mauaji, majeraha, uharibifu wa mali na upotevu wa maisha uliotokana na vurugu hizo.
“Haya mauaji yametuacha tukiwa tumejeruhiwa wote. Tunatoa pole nyingi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao,” amesema.
Amesema TEC inaendelea kuwaombea majeruhi wapone na kurejea katika shughuli zao, huku ikiwafariji wale walioathirika kiroho, kisaikolojia na kiuchumi.
Ametoa wito kwa mamlaka kulaani mauaji hayo na kukiri kwamba waathiriwa ni sehemu ya jamii ya Watanzania.
Amesema Tume huru isiyofungamana na upande wowote inahitajika ili kuliponya Taifa, ambayo itajumuisha taasisi za kimataifa, za dini, asasi za kiraia na wataalamu wa masuala ya haki na demokrasia.
Aidha, ameishauri Serikali kuwa tayari kupokea maoni ya ripoti itakayotolewa, akisema hilo linaweza kuwa hatua muhimu ya kusaidia uponyaji wa Taifa linapoelekea kwenye maridhiano.
“Wote waliokamatwa kwa hila kabla na wakati wa uchaguzi waachiwe huru bila masharti yoyote,” amesema Askofu Pisa.
Pendekezo hilo, limetolewa wakati kuna maelekezo ya Rais Samia kwa vyombo vya sheria, hususan Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, kuangalia makosa ya vijana waliokamatwa na kuwapunguzia au kuwaondolea mashtaka wale ambao hawakuonyesha dhamira ya kufanya uhalifu bali walifuata mkumbo.
TEC pia imesisitiza ulazima wa kuanza mchakato wa Katiba mpya, ikibainisha kwamba ni kilio cha muda mrefu cha Watanzania.
“Katiba mpya inapaswa kujali utu, usawa na ukweli kwa wote. Tusikilize wananchi ili tusirudi kwenye machafuko,” amesema Askofu Pisa.
Sheikh Ponda: Haki, uadilifu
Katibu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda amesema maridhiano hayawezi kuwa na tija ikiwa hayatakabili kwa uwazi chanzo cha migogoro na madhara yaliyotokea. Amesema misingi ya haki na uadilifu ndiyo msingi wa kujenga jamii iliyoungana.
“Maridhiano yanaweza kutatua changamoto endapo yatakuwa ya kweli, yasiyoegemea upande mmoja na yatakayowashirikisha wadau wote muhimu,” amesema Sheikh Ponda.
Mbali na hilo, Sheikh Ponda amezungumzia uchaguzi mkuu, akisema utafiti wao umebaini kuwa mchakato wa uchaguzi, kuanzia uandikishaji wa wapiga kura, upigaji kura hadi kutangazwa kwa matokeo, ulikumbwa na dosari zilizojitokeza wazi.
Kwa mujibu Ponda, changamoto hizo zinaonyesha hitaji la mabadiliko ya dharura katika mifumo ya uchaguzi na uwajibikaji wa taasisi za dola.
Ameongeza kuwa kasoro hizo zimeathiri sura ya uchaguzi na kupunguza imani ya wananchi katika mchakato huo, ikiwamo kutokea kwa vurugu katika baadhi ya maeneo na taarifa za vifo vya raia vilivyotokana na vurugu hizo na wengine kujeruhiwa na kutojulikana walipo.
“Tunalaani mauaji hayo. Tunatoa salamu za rambirambi kwa familia zote zilizoondokewa na wapendwa wao, tukitumaini kuwa amani itarejea nchini,” amesema.
Vilevile, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe amesema maridhiano yanapaswa kuanzia katika kutambua kiini cha tatizo.
Ametaka mchakato uwe shirikishi kwa kiwango sawa na ule wa Bunge Maalumu la Katiba ili kutoa nafasi kwa wananchi kutoa maoni yao. Ameonya kuwa kushindwa kwa maridhiano kati ya Serikali na Chadema mwaka 2024 kunapaswa kuwa fundisho muhimu la kuepuka kurudia makosa.
“Maridhiano haya lazima yaangalie mbele na yashughulikie chanzo cha tatizo kwa uwazi. Lazima wananchi wasikilizwe kwanza kabla ya hatua za maridhiano kufikiwa,” amesisitiza.
Makamu Mwenyekiti wa NCCR–Mageuzi (Bara), Joseph Selasini, amesema maridhiano ya kweli hayawezi kufikiwa bila kufanyika uchunguzi huru kuhusu matukio ya vurugu na mauaji yaliyotokea nchini.
Amesema mchakato wowote unaolenga kuunganisha Watanzania unapaswa kuanzia kwenye ukweli wa kilichotokea, hatua ambayo tayari Rais Samia ametangaza kuwa Serikali inaichukua kupitia Tume maalumu ya uchunguzi.
“Kufanya maridhiano ni kuridhiana nini, na nani?” amehoji Selasini akisisitiza kuwa msingi wa maridhiano ni kujadili kwa uwazi kinachowagawa wananchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa NRA, Hassan Almas amepongeza nia ya kuanzisha maridhiano na kusisitiza kuwa mchakato huo unapaswa kuwahusisha wadau wote muhimu. Hata hivyo, ameshangazwa na wito wa baadhi ya watu kutaka uchunguzi ufanywe na wadau wa nje ya nchi.
“Napongeza juhudi za kutafuta maridhiano, ni hatua nzuri. Lakini niombe tusifikie hatua ya taasisi au mtu yeyote kususia,” amesema Almas.
Katika hatua nyingine, Jumuiya ya Umoja wa Wazazi ya CCM imepongeza hatua ya Rais Samia ya kuwasamehe vijana waliokamatwa katika vurugu za Oktoba 29.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Maganya Rajabu amewataka vijana kuacha kufuata kila kinachoibuka mitandaoni, akisema msamaha huo unaonyesha ukomavu wa kisiasa na moyo wa huruma.
“Sote ni mashahidi kwamba nchi nyingi zimepitia machafuko ya aina hii lakini hazikuchukua hatua kama hii ya Rais ya kuwasamehe vijana. Huu si uoga, ni ukomavu wa kisiasa,” amesema Manganya.