Wabuni mfumo masoko ya mazao kudhibiti madalali

Arusha. Taasisi ya Sotech imetengeneza mfumo wa kisasa wa kusaidia wakulima kuuza mazao yao kwa njia ya mtandao, ili kusaidia wakulima kuondokana na changamoto ya soko na ukosefu wa taarifa zake sahihi.

Mfumo huo ujulikanao kama Kikapu, umeanzishwa kuwasaidia wakulima kuunganishwa na masoko moja kwa moja pamoja na uhifadhi wa taarifa za mauzo kwa wakulima, ili kuwasaidia kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha.

Katika mahojiano na Mwananchi Novemba 12, 2025 na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Awadhi Massomo amesema tangu mwaka 2023 hadi sasa wamefanikiwa kuunganisha wakulima, kusaidia ununuzi wa pembejeo, mawasiliano na maafisa ugani na taasisi za kifedha.

“Mpaka sasa tumeshasaidia wakulima zaidi ya 100 kuwaunganisha na masoko na moja ya changamoto kubwa tuliyobaini ni wakulima wengi hawana elimu ya utumiaji wa simu janja, hivyo tunaendelea kutoa elimu ya matumizi ya simu janja na kutumia mifumo kufanya biashara,” amesema.

Kuhusu mikopo amesema katika tafiti walizofanya kwenye taasisi nyingi za fedha, miongoni mwa masuala waliyobaini ni wakulima wengi kutokuwa na taarifa sahihi za uuzaji wa mazao, hivyo kwa sasa tunawaelekeza kutumia mifumo kutunza taarifa zao ili wakopesheke.

“Tumejaribu kuongea na taasisi za fedha na kuangalia wanavyotoa mikopo, changamoto ni wakulima wengi kupika taarifa za uuzaji, kwa hiyo tunawaelimisha watumie mifumo kuhifadhi taarifa zao,” alisema.

Alisema kupitia mfumo wa kikapu unamsaidia mkulima kuweka taarifa zake kupitia simu janja na anaandika amelima kiasi gani na anatarajia kuvuna kiasi gani, akija kuvuna wanalinganisha na kuona kile kiwango alichokadiria na alichokipata.

Massomo alisema kwa sasa kupitia mfumo huo wameanza na mazao ya mbogamboga, maua na matunda kwa kuwa uhitaji wake ni mkubwa lakini pia ni mazao yanayoharibika kwa haraka, hivyo wakulima wengi hushindwa kuyahifadhi.

“Mazao hayo yamepata wasindikaji wadogo wengi, hivyo tumeona ni fursa kwa wakulima na ndiyo maana tunawasaidia ili wapate masoko ya moja kwa moja kuepuka madalali ambao kwa kiasi kikubwa walikuwa wanawarudisha nyuma,” amesema.

Massomo anaongeza kuwa kwa sasa wameanza na mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Dodoma pamoja na Pwani (Bagamoyo) ambapo wameanza kuchakata takataka zitokanazo na mazao hayo, yakiwamo maganda ya mayai ambayo yakishachakatwa huuzwa kwa wakulima kama mbolea.

Amesema wamekuwa wakishirikiana na Serikali ikiwamo Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), ambapo wameanza kufanyia kazi kwa kutengeneza mfumo ambao utakuwa na uwezo wa mkulima kuwasiliana na ofisa ugani kwa njia ya mtandao.

“Mfumo utamwezesha mkulima kupiga picha zao lake lenye changamoto akatuma kwenye mfumo na bwana shamba akaona na kumweleza ni changamoto gani na atumie dawa gani, tunaendelea kuangalia namna ya kutatua kupitia teknolojia,” anasema.

Mmoja wa wakulima wa viazi kutoka Forest, wilayani Arumeru, Mariana Joseph amesema mfumo huo ukiwafikia utaweza kuwasaidia kuuza mazao yao kwa njia ya mtandao bila kuingiliwa na madalali, ambao mara nyingi wanapandisha bei ya mazao na kuwaweka katika hali ngumu.

Amesema kuwa mfumo huo utasaidia kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo hasa kwa kuongeza uwazi na kupunguza urasimu katika uuzaji wa mazao yao.

“Sisi wakulima mfumo huu ukitufikia sote utatuondolea adha ya kutafuta masoko, tutaondokana na madalali ambao wamekuwa wakinufaika na sisi wakulima kubaki na hali duni.”