Wadau walivyopokea ahadi ya Samia ajira za walimu

Dar es Salaam. Wimbi la msongamano katika shule za msingi na sekondari nchini limepata mwelekeo mpya, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza ajira 7,000 za walimu zitakazotolewa ndani ya siku 100 za kwanza za Serikali anayoiongoza.

Hata hivyo, wadau licha ya kupongeza hatua hiyo, wana hofu ya uhimilivu wake kwa miaka ijayo na hata ugawanywaji wa walimu hao.

Ahadi ya Rais Samia imekuja wakati malalamiko kuhusu ongezeko kubwa la wanafunzi darasani yakizidi kushika kasi, huku baadhi ya shule zikiripotiwa kuwa na wanafunzi 300 hadi 500 kwa darasa moja, hali inayotajwa kuathiri kwa kiasi kikubwa ubora wa elimu.

Akizungumza jana wakati akilifungua Bunge la 13 jijini Dodoma, Rais Samia amesema Serikali imejipanga kupunguza mzigo mkubwa waliokuwa wakibeba walimu kwa miaka mingi kutokana na uhaba wa watumishi wa elimu.

“Serikali tayari imetangaza ajira 7,000 za walimu. Hii ni hatua ya mwanzo kujibu kiu ya wananchi ya kuboresha elimu,” amesema Rais Samia, akibainisha kuwa ajira hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali kuboresha miundombinu na kufanya sekta ya elimu iwe na tija zaidi.

Licha ya hatua hiyo kupongezwa, wadau wa elimu wanasema juhudi hizo bado hazitoshi kugusa kwa kina mizizi ya tatizo la msongamano, hasa kwenye maeneo ya mijini na pembezoni ambako idadi ya wanafunzi imeongezeka maradufu kufuatia mpango wa elimu bila ada ulioongeza mwamko wa wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni.

Akizungumza na Mwananchi, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, (MUM) Hamad Msamaa, amesema tatizo la ajira kwa vijana ikiwemo walimu, haliwezi kutegemea Serikali pekee.

“Kutokana na maeneo mengi niliyotembelea, sehemu yenye uwezo mpana wa kupanua ajira ni sekta binafsi. Ukijengwa uhusiano mzuri kati ya Serikali na sekta binafsi, tatizo la ajira linaweza kumalizika au kupungua kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Msamaa ameongeza kuwa mfumo wa elimu unahitaji mabadiliko ya kimwelekeo kutoka kwenye elimu ya kukariri kwenda kwenye elimu ya ujuzi.

“Elimu ya ujuzi ndiyo itakayomjengea kijana uwezo wa kujitegemea. Lazima tuondokane na mfumo wa kuhifadhi maarifa bila kuyatumia. Vitendo viwe msingi wa elimu yetu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali itaharakisha ujenzi wa shule mpya, kuongeza madarasa na kukarabati miundombinu ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi.

“Tunaenda kuwekeza kwenye shule mpya za awali, msingi na sekondari pamoja na kuongeza madarasa kwenye shule zilizopo,” amesema Rais Samia, akisisitiza kuwa mpango huo ni sehemu ya ajenda ya Taifa ya kuinua elimu.

Kwa upande wa walimu, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Dk Seleman Ikomba, ameipongeza Serikali kwa kutangaza ajira hizo, akisema ni “faraja kwa walimu ambao wamekuwa wakibeba mzigo usiostahimilika.”

“Tumeona mwelekeo wa mahitaji ambayo tumekuwa tunayapigia kelele yakifanyiwa kazi hatua kwa hatua,” amesema Dk Ikomba.

Amesema zipo shule za msingi zenye mwalimu mmoja anayefundisha darasa la pili hadi la saba, hali inayomchosha mwalimu na mwishowe kuathiri ubora wa elimu.

“Hata sekondari, utakuta mwalimu mmoja wa hisabati anafundisha kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne. Huu ni mzigo mkubwa na si wa kawaida. Mwalimu ni binadamu, lazima achoke,” amesema.

Dk Ikomba ametaja pia umuhimu wa ajira hizo kuelekezwa katika maeneo maalumu.

“Kuna dhana kuwa mijini hakuna uhaba wa walimu, lakini kwasababu ya wingi wa wanafunzi, mijini nako kunahitaji walimu wengi zaidi. Hata hivyo, mikoa ya pembezoni kama Mtwara, Lindi, Katavi, Rukwa na Kigoma ndiyo yenye uhaba mkubwa zaidi,” amesisitiza.

Kwa upande wao, wazazi wamelalamikia msongamano, wakisema unadidimiza ubora wa elimu wakisema mwalimu mmoja hushindwa kuwafuatilia wanafunzi wote.

“Tunahitaji walimu wa sayansi fizikia, kemia na hesabu. Ndiko upungufu uko kwa kasi kubwa. Bila kuimarisha eneo hili, hatutafika mbali,” amesema mama Flora, mzazi wa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Wadadisi wanaamini ajira 7,000 ni hatua ya maana, lakini wanataka mpango mpana zaidi wa kudumu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliyeomba kutotajwa jina, amesema: “Hatua hii ina mantiki, lakini hatuwezi kupunguza msongamano bila kuwa na mpango wa miaka mitano wa ajira za walimu. Ajira za kila mwaka zikisimama, tatizo litarudi pale pale.”

Wadau pia wameshauri kuanzishwa kwa kanzidata ya kitaifa ya mahitaji ya walimu, ili kuwezesha upangaji wa rasilimali watu kwa usawa kulingana na uhitaji halisi wa shule.

Kwa ujumla, mwelekeo wa Serikali umeamsha mjadala mpya kuhusu mustakabali wa elimu, miundombinu na uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi. Lakini maswali bado yanasikika mtaani na kwa wadau wa elimu: Je, ajira 7,000 ni suluhisho la muda mfupi, au ni mwanzo wa hatua za kudumu za kuondoa msongamano shuleni?