KOCHA Mkuu wa Alliance Girls ya Mwanza, Sultan Juma amesema kikosi chake kiko vizuri na kimefanya maandalizi ya kutosha jambo linakompa imani watafanya vyema katika Ligi Kuu ya Wanawake Bara na kumaliza nafasi nne za juu.
Alliance Gilrs itacheza mechi ya kwanza ya WPL keshokutwa Jumatano dhidi ya Ceassia Queens kwenye Uwanja wa Nyamagana, baada ya mchezo uliopaswa kuchezwa Ijumaa dhidi ya Fountain Gate Princess kuahirishwa.
Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo, Juma amesema msimu uliopita walimaliza nafasi ya tano lakini msimu huu wanataka kupanda juu wakilenga kumaliza katika nafasi ya nne hadi ya kwanza kwa kuchukua ubingwa.
“Mwaka huu tumejipanga na tuko vizuri, maandalizi yetu yanaendelea vizuri wachezaji wote wako sawa timu nzima kwa sasa hatuna mwenye shida, hivyo naweza kuwathibitishia mashabiki wetu tupo vizuri mwaka huu,” amesema Juma.
Amesema timu yake ambayo ni matunda ya kituo cha michezo cha Alliance kilichopo Mahina, Mwanza wamefanya mchujo wa vijana wao na kutengeneza timu nzuri ambayo itaibua nyota wa baadae katika soka la Tanzania.
“Mwaka jana tulimaliza katika nafasi ya tano, mwaka huu tunahitaji tuongeze kidogo tusogee juu kuanzia nafasi ya nne, ya tatu, pili na hata ubingwa, kwahiyo tumejipanga vizuri ili tufanye vizuri mwaka huu,” alisisitiza kocha huyo.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Alliance Girls, Simon Kabwema amesema;
“Sisi kama Alliance Girls tunaendelea na maandalizi mazuri timu ipo vizuri morali ni kubwa, mechi yetu dhidi ya Ceaasia Queens tunawaahidi kwamba timu yetu itaondoka na ushindi na kuanza vyema msimu huu.”