KOCHA Mkuu wa KenGold, Jumanne Challe amesema licha ya mwenendo mzuri hadi sasa, ila anakabiliwa na changamoto kubwa ya kubadilisha wachezaji nafasi zao wanazocheza, kwa sababu kikosi hicho kina nyota wanane wanaocheza namba nane uwanjani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Challe amesema katika wachezaji wanaocheza namba nane, wapo wanane katika timu hiyo msimu huu, hivyo kazi anayoifanya ni kuwabadili baadhi yao, ili tu kuendana na mahitaji kwa sababu ya ufinyu wa kikosi.
“Timu imefungiwa madirisha matatu ya kutosajili na wachezaji waliopo ni wadogo na wanahitaji muda sana wa kuzoeana, sasa ukiangalia wanaocheza nafasi moja ni wanane uwanjani, ni kazi kubwa kwa benchi la ufundi kuwabadilisha,” amesema Challe.
Timu hiyo iliyocheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, ilianza kufundishwa na Kocha Fikiri Elias, kisha kuteuliwa Omary Kapilima akisaidiana na Jumanne Challe walioiongoza hadi mwisho mwa msimu, licha ya ujio pia wa Mserbia Vladislav Heric.
Kwa msimu wa 2023-2024, KenGold ilitwaa ubingwa wa Championship, ikiibuka kinara na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 67, iliyorejea Ligi Kuu baada ya miaka 21, tangu iliposhuka mwaka 2001.
Licha ya kiwango hicho, ila KenGold ilishindwa kumudu presha za Ligi Kuu na msimu wa 2024-2025, iliburuza mkia na pointi 16, ikishinda mechi tatu tu, sare saba na kupoteza 20, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza nafasi ya 15 na pointi 23.