Katika ulimwengu wa uhusiano wa kimapenzi, si jambo geni kusikia au kushuhudia mwenza akiachana na mpenzi wake na kisha kurudi baada ya wiki, miezi au hata miaka.
Lakini ni nini hasa humsukuma mwenza kurejea kwenye uhusiano aliouacha mwenyewe? Je, ni mapenzi ya dhati au ni mazoea tu yanayomrudisha? Mara nyingi, watu hugundua thamani ya kitu fulani baada ya kukipoteza. Vivyo hivyo, mwanaume anaweza kushindwa kuona wazi wema, uaminifu, na upendo wa mpenzi wake hadi pale anapokosa uwepo wake.
Katika ukimya na upweke, huanza kukumbuka mambo mema aliyokuwa akipata, maneno ya faraja, mapishi mazuri, usikivu, au hata msaada wa kihisia.
Kama walivyosema wahenga, “Samahani huja baada ya majuto.” Wengine hurudi wakijuta na kuomba msamaha, wapenzi wao wawape nafasi nyingine.
“Wanaume wengine hurudi kwa sababu wanajuta kuondoka labda walikuwa wakali, walikosea kwa maneno au vitendo, au waliamua kuondoka kwa pupa bila kufikiria. Majuto ya kweli huweza kumfanya mwanaume atafakari na kuona haja ya kurudi kurekebisha makosa yake,” anasema mtaalamu wa mapenzi, Jones Kioko kama alivyonukuliwa katika mtandao wa gazeti la Taifa Leo.
Anasema katika hali kama hizi, mwanamume kurudi kwake huwa ni njia ya kuomba msamaha, na pengine kutaka kuanza ukurasa mpya kwa uhusiano wenye afya.
Mtaalamu huyu anasema wengine hurudi si kwa sababu ya mapenzi, bali kwa sababu ya upweke.
“Kwa vile huwa wamezoa kuwa na mtu wa karibu wa kuongea naye, kushirikiana naye, au hata kushikana mikono. Wanapokosa hali hiyo, hujipata wakimkumbuka yule waliyemuacha,” anaeleza Kioko.
Cidy Wairimu, mtaalamu wa masuala ya uhusiano anasema hapa ndipo tahadhari inahitajika, maana kurudi kwa sababu ya mazoea au faraja ya muda si sawa na kurudi kwa sababu ya upendo wa kweli. Mtu anaweza kurudi kwa sababu ya hali, sio hisia.
“Wakati mwingine mwanaume humwona mwanamke aliyemuacha akiendelea mbele, akifurahia maisha, amepata mpenzi mwingine au anang’ara zaidi kuliko awali. Hali hii huweza kuamsha hisia za wivu au hofu ya kumkosa kabisa,” anasema.
Kwa sababu hiyo, anaeleza, mwanamume kama huyu hurudi si kwa sababu amejifunza au amebadilika, bali kwa sababu hataki kuona mwingine akifurahia kile alichokipoteza.
Hata hivyo, si wenza wote hurudi kwa sababu mbaya. Kuna baadhi wanaotafakari, kujifunza kutokana na makosa, na kubadilika kwa dhati. Wanaweza kuwa wamepitia kipindi kigumu cha maisha kilichowasaidia kukua kiakili, kihisia na kiroho.
Kwa wenza wa aina hii, kurudi ni ishara ya mtu aliyejifunza na anayetaka kujenga upya kwa misingi bora.
Wakati mwingine, hisia za ndani kati ya wawili hao huwa bado zipo. Mapenzi hata yakififia, hayawezi kufutika kwa haraka. Mwenza anaweza kurudi kwa sababu bado anampenda mpenzi wake wa zamani na ameshindwa kuunganisha moyo wake kwa mwingine.
Hisia hizo ni kama mvuto wa sumaku unaomrudisha polepole, hata baada ya majaribio ya kusahau au kuendelea mbele.
Sababu nyingine inaweza kuwa ni mambo ya nje ya uhusiano kama vile familia, marafiki, au mabadiliko ya maisha. Huenda familia yake ilimshauri arudi, au marafiki walimfungua macho kuhusu kilichomponyoka.
Katika baadhi ya hali, Wairimu anasema mwanaume hurudi si kwa sababu ya mapenzi bali kwa sababu ya mashinikizo au hali fulani ya maisha inayomfanya kurudi mahali alipozoea.
Anasema kwamba kumrudia mpenzi wa zamani ni uamuzi wa kina unaohitaji hekima. Si kila mwanaume anayekurudia ana nia njema.
Kwa wewe ambaye mwenza wako ameomba ‘kurudisha majeshi’, kabla ya kumpokea, jiulize: Je, sababu yake ya kurudi ni ya kweli au ni ya muda?Je, ametambua makosa na yupo tayari kubadilika?
Aidha, moyo wako uko tayari kumkumbatia tena au unapaswa kuendelea mbele?
“Akirudi kwa moyo wa toba, akiwa amekomaa na anataka kujenga upya, basi anaweza kupewa nafasi. Lakini kama amerudi kwa sababu ya wivu, mazoea au hofu ya kukupoteza, basi tafakari kwa makini kabla ya kufanya uamuzi,” anasema Kioko.