Dk Bashiru: Tumepiga hatua kidemokrasia, lakini umaskini bado

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amesema pamoja na hatua zilizopigwa kidemokrasia, Tanzania bado haijafanya vizuri katika eneo la haki ya jamii.

Katika ufafanuzi wake, Dk Bashiru amesema haki ya jamii inahusisha umaskini alioutaja kuwa kikwazo cha kupata makazi, ulinzi wa mali na hata uhuru wa kuzungumza.

Mwanazuoni huyo wa sayansi ya siasa aliyeteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mbunge, amepinga hoja kuwa, CCM inazalisha vyama pinzani kushindana navyo, akisema hiyo ni kuvidharau vyama hivyo.

Dk Bashiru amesema hayo alipohojiwa katika kipindi cha Medani za Siasa, kilichorushwa na Televisheni ya Mtandaoni ya Jambo, Novemba 13, 2025.

Alipoulizwa ni eneo gani Tanzania halifanyi vizuri kwenye nyanja ya demokrasia, Dk Bashiru ametaja suala la haki ya jamii.

Amedokeza wakati hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akipambana kupata uhuru na kujenga Taifa jipya, nchi ilikuwa inakabiliana na maadui watatu yaani ujinga, umaskini na maradhi.

Amesema katika mazingira ambayo hujafanikiwa vema kupambana na maadui hao, huwezi kusema demokrasia imekamilika.

Amesisitiza maadui hao ndio wanakwaza watu kupata haki zao ikiwamo ajira, makazi bora na ulinzi wa mali zao, hivyo eneo muhimu la kujipanga kukabiliana nalo ni kukomesha umaskini.

“Eneo ambalo tunapaswa kuongeza nguvu ni eneo la haki za kijamii. Jamii kuwa na uhakika wa chakula, kila mtu kuwa na uhakika wa chakula, malazi bora na kila mtu kuwa na sauti,” amesema Dk Bashiru ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Alipoulizwa iwapo anaiona demokrasia inasonga mbele au inarudi nyuma, amesema inasonga mbele pamoja na upungufu katika taasisi za kidemokrasia uliopo bayana.

Dk Bashiru amesema bado Tanzania ni moja na ina utulivu na amani, huku taasisi za kidemokrasia zinaendelea kukomaa, akisisitiza kuna kazi kubwa ya kukomaza demokrasia.

Akijibu kuhusu wakosoaji wa demokrasia ya Tanzania, Dk Bashiru amesema hayo ni maoni na yanazungumzwa hata ndani ya nchi.

Amesema watu wanapaswa kutofautisha demokrasia ya nchi moja na nyingine, kwa kuwa, mapambano ya kudai uhuru, haki kutoka kwa jamii moja hadi nyingine mara zote hayako sawa.

“Kila jamii kwa namna mbalimbali inaweza kuendesha mchakato wa pambano wa kujikomboa na kujitawala kwa namna tofauti, kwa hiyo hata anayekuja kukosoa lazima azingatie mambo hayo.

“Simaanishi jamii moja haiwezi kujifunza kutoka jamii nyingine, kwa sababu jamii isiyojifunza ni ya kipumbavu, yapo maeneo unaweza kujifunza kutoka jamii iliyofanya vizuri kwenye mchakato huo,” amesema.

Pia, amesema yapo maeneo mengine ambayo huwezi kuyafanya kwa sababu hayafanani na jamii yako, hivyo ni vizuri wanaokosoa wazingatie hayo.

Hata hivyo, Dk Bashiru amesema hamaanishi mfumo wa demokrasia nchini upo sahihi au kamili, kwa kuwa unawahusisha watu, lazima kutakuwa na makosa ya kusahihisha na mambo mapya ya kujifunza.

Amesema kwa vipimo vya Tanzania, demokrasia ipo, lakini sio kamili bali inatakiwa kuimarishwa misingi yake na kukomazwa kiutamaduni na tabia.

Amesisitiza hakuna namna ya kusema demokrasia imekamilika japo ipo kwa namna ya kuridhisha.

Kuhusu uhuru wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Dk Bashiru amesema wa chombo hicho unahusisha mambo mengi, ikiwamo uwezo wake wa kusimamia mambo yake kwa gharama zake na kuwa na uamuzi bila kuingiliwa.

Amesema INEC ni chombo huru kwa sababu hata kwenye uchaguzi wa mwaka huu, imetumia fedha za ndani kuendesha uchaguzi na haikuingiliwa kwenye uamuzi wake.

“Kujitawala ni kujitegemea, msingi mkubwa wa demokrasia ni uhuru na uhuru ni uwezo wa kuendesha mambo yako bila kuombaomba au kusaidiwa na watu ambao misaada yao inaweza kuambatana na masharti,” amesema.

Dk Bashiru amesema madai ya INEC kutokuwa huru na inaipendelea CCM yanatoka kwa watu ambao hawafanyi vizuri kwenye uchaguzi na wangefanya vema wasingelaumu.

Amesema suala la ushindani mara nyingi lina malalamiko na ndio maana ni vizuri kuwepo kwa fursa anayelalamika kwenda mahakamani kutetea hoja yake na kupata haki yake.

Upinzani kudaiwa mradi wa CCM

Alipoulizwa kuhusu ushindi wa asilimia 97.6 wa Rais Samia, Dk Bashiru amesema mwaka 1995 hadi 2000 Chama cha NCCR Mageuzi kiliibuka kuwa chama kikuu cha upinzani lakini hakikuitwa mradi.

Vivyo hivyo, amesema kwa CUF ilikuwa inafanya vema Tanzania bara na Zanzibar haikuitwa mradi wa CCM, lakini kuanguka kwao kumesababisha viitwe majina hayo.

“NCCR ambayo imewahi kuwa chama kikubwa cha upinzani na zamu hii imeshiriki pia kwanini leo iitwe project na sio mwaka ule uliokuwa chama kikuu cha upinzania.

“Mimi nadhani kwanza ni kuvidharau na kudhalilisha vyama ambavyo vimeanzishwa na Watanzania kwa haki yao na kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Dk Bashiru amesema CCM imeenea Tanzania bara na Zanzibar, hivyo haina sababu ya kuanzisha vyama mradi na hakukuwahi kufanyika kikao kilichoazimia kutengeneza chama mradi.

Alipoulizwa kuhusu maandamano yaliyozaa vurugu Oktoba 29, amesema kuna vitu vilikuwa vinajadiliwa kuashiria tayari kulikuwa na mjadala wa mambo ambayo nchi inaweza kufanya kuwaleta watu pamoja.

Amesema masuala la maridhiano na kusuluhishana yalikuwepo hata kabla ya uchaguzi.

Akirejea namna Rais Samia alivyoingia madarakani Machi 19, 2021 baada ya mtangulizi wake, Rais John Magufuli kufariki dunia Machi 17, 2021 na kuapishwa kwa mujibu wa Katiba kushika mamlaka hayo, Dk Bashiru amesema ni wakati ambao Taifa liliathiriwa na Uviko-19 na kulikuwa na hali ya kutoaminiana.

“Zipo hatua zilichukuliwa ikiwamo kuwaachia watu waliokuwa na kesi za kisiasa, kuruhusu shughuli za kisiasa, kufanyika mazungumzo ya marekebisho ya mfumo wa kidemokrasia na uchaguzi hatua iliyosababisha kuundwa kwa kikosi kazi,” amesema.

Alipoulizwa kama kungefanyika maridhiano kabla ya uchaguzi Oktoba 29 huenda madhara yaliyotokea yasingetokea, Dk Bashiru amesema mazungumzo yalifanyika.

Amesema baadhi ya maazimio hayo yalitekelezwa kwa kurekebisha sheria za uchaguzi na kurekebisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo sasa ni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

“Katika mazingira hayo, yapo mambo yasingeweza kukamilika ikiwamo suala la Katiba mpya, ndiyo maana baadhi ya mambo yanazungumzwa kufanyika baada ya uchaguzi,” amesema.