George Mpole anasikilizia simu tu

NYOTA wa zamani wa Geita Gold na Pamba Jiji aliyewahi kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, George Mpole amezungumzia ukimya wa muda mrefu alionao kwa kufichua alikuwa akifanya majaribio na klabu ya Siwelele F.C iliyopo Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Mpole amesema majaribio hayo yalikuwa ya takriban wiki tatu wakati ligi ya nchi hiyo ikiwa inaendelea, hivyo walitaka kuwaangalia wachezaji watakaowaongeza dirisha dogo la usajili na kwa sasa amesharudi nchini akisikilizia mchongo.

“Nimerejea wiki mbili zilizopita baada ya kumaliza kufanya majaribio hayo, kama watanihitaji watanipigia simu, ikishindikana nitaendelea na mambo mengine, kwa sababu dirisha dogo la usajili litakuwa limefunguliwa maeneo tofauti,” amesema Mpole na kuongeza;

“Katika majaribio hayo tulikutana wachezaji wengi kutoka mataifa mbalimbali na kilichoongezeka kwangu ni kujiamini na uthubutu wa kuendelea kupambana nje ya mipaka ya Tanzania.”

Mpole aliyewahi kuibuka mfungaji bora wa mabao 17 msimu wa 2021/22, amesema mpira wa miguu ni kazi yake anatambua anapokuwa hana timu kitu gani akifanye ili kulinda kiwango chake.

“Nimejiwekea misingi bora ya kujisimamia kufanya mazoezi ya kuhakikisha nakuwa fiti, nina programu ninayoifuata kila siku labda itokee niumwe, ndipo nitapumzika,” amesema Mpole aliyewahi kuzichezea Pamba, Geita na Mbeya City.