Kile kinachodharauliwa, Mungu hukitukuza | Mwananchi

Tumsifu Yesu kristu. Tunakusalimu kwa Jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai. Ninamtukuza Mungu kwa ajili yako kwa kuendelea kuachilia neema ya uhai kwako na kwa familia yako. Ni imani yangu kuwa unaendeleaa vizuri katika safari hii ya kuutafuta uso wa Mungu. Mungu akubariki sana.

Tunakukaribisha kuungana nasi katika tafakari ya ujumbe wa leo unaosema, Kile kinachodharauliwa Mungu hukitukuza”.

Naamini ujumbe huu umekuja mahususi kabisa kwa ajili yako na ni maombi yatu kwa Mungu kuwa ujumbe huu utafanyika uponyaji kwako lakini pia utapata nafasi ya kuweza kuwasaidia wengine. Bwana yesu asifiwe.

Dharau ni dhana pana kiasi, kwa mujibu wa Kamusi ya Tuki (2004) neno dharau linamaana ya kuwa na hali ya kukosa kuthamini mtu, kitu; vunjia mtu heshima, au kutotilia maanani.

Ni tabia ya kutothamini au kutoheshimu mtu au kitu, tabia ya kupuuza. Hebu tusome katika Biblia kitabu cha Yohana 1:45-50. Ni habari za Yesu akijijengea timu atakayofanya nayo kazi ya injili hapa duniani. Mistari hiyo tuliyoisoma inahusu Filipo na Nathanaeli wakiitwa na Yesu ili wawe wafuasi wake.

Kabla hatujaendelea, naomba tukueleze kidogo kwa ufupi sana habari za mji wa Nazareti. Mji wa Nazareti kwa macho ya kibinadamu ulikuwa ni mji au eneo lisilotegemewa jambo jema kutokea huko. Ni eneo duni sililovutia watu wa maana kuishi huko. Kwa lugha ya sasa hivi tunaweza kuliita “Eneo lililosahaulika”. Kwa namna ilivyotegemewa ilikuwa Yesu azaliwe katika miji mikubwa yenye hadhi na ya kuvutia kwa sababu yeye ni Mfalme. Kuna jambo la kujifunza kuhusu Nazareti:

Nazareti ulikuwa mji walioishi watu masikini na duni kabisa kabla ya ujio wa Yesu. Palikuwa eneo ambalo lilijaa umasikini  usiotamanika.

Nazareti haukuwa mji wenye kuvutia wala umaarufu, hapakuwa na jambo lolote la maana katika mji huu. Watu wake hawakupata elimu nzuri wala pesa za kutosha

Nazareti ulikuwa mji ambao ulikuwa na watu wasiokuwa na matumaini. Kila aliyetamani kuingia Nazareti hakujisikia vizuri.Wakazi wa mji huo hawakuwa na matumaini kabisa, walikata tamaa kwa sababu ya sifa mbaya ya mji huo.

Nazareti ni mji alikolelewa Yesu na wazazi wake walikuwa watu duni sana. Ndiyo maana hata Mariamu mwenyewe alipoambiwa habari ya kuchukua mimba na kumzaa Masihi wa Mungu, alishangaa na kutokuamini kabisa habari ile kwa kuangalia hali yake ilivyoduni kabisa.

“Laweza neno jema kutoka Nazareti?” hili ni swali la kushangaza sana. inawezekana Nathanaeli aliujua mji wa Nazareti vizuri na vituko vyote ndani ya mji huo. Hii kauli ndani yake ukiichunguza utagundua kuwa kuna dharau ya kutosha juu ya mji wa Nazareti na wote wanaokaa humo.

Inawezekana kabisa kuna mambo mengi yanayokuzunguka na mambo hayo yamepelekea kudharaulika na kutopewa heshima yako kama unavyostahili. Inawezekana unatoka kwenye familia duni au yenye historia Fulani mbaya katika jamii, inawezekana kazi unayoifanya haikupi heshima, kipato ni kidogo, inawezekana mji/kijiji/mtaa uliopo hauna historia nzuri. Inawezekana unapitia mazingira magumu hata kwenye ndoa yako na hata heshima ya kuwa baba au mama wa familia unaikosa. Je, Watu wanaokuzunguka wanakudharau kupita kiasi na unajisikia vibaya kuendelea na kazi au hiyo ndoa? Je, unapitia wakati mgumu kupata mke au mume bora kwa sababu ya historia ya familia yako au hali yako ya kiuchumi? Inawezekana kila anayekuja mnajiandaa hata wazazi wanajua sasa kijana au binti yetu amepata mwenzake lakini baada ya muda mfupi mambo yanaharibika na hata hutaki tena kusikia sauti yake.

Je, inawezekana watu wanakusema sana na kukushambulia vibaya katika eneo la kazi au kwenye familia yako kwa sababu wakitazama historia yako na kile unachokifanya vinatofautiana yaani wewe kazi yako ni bora zaidi kuliko zao?

Bwana Yesu ametutuma tukutie moyo kwamba usikate tamaa. Inawezekana ukisikiliza historia za watu wanaokuzunguka namna walivyo wakuu na wanatoka kwenye familia zenye hadhi ukilinganisha na wewe unajikuta unakata tamaa kupita kiasi.

Yote yanawezekana kwake yeye aaminiye, ukiendelea kumwamini Kristo kupitia ujumbe huu inawezekana kabisa ukabadilisha maisha, ndoa, mtazamo kazini na katika jamii.

Badala ya kuonekana duni ukaonekana bora zaidi kwa sababu Mungu akutiaye nguvu yumo ndani yako. Usikate tamaa, haijalishi wanaongea nini juu yako, eti tuone kama ataoa au kuolewa, tunakutia moyo ya kwamba jambo jema lipo mbele yako na litatokea kwako usirudi nyuma.

Unaweza kuamua leo kupitia mtazamo wako, mwenendo wako au hata kauli zako ya kwamba jambo jema ambalo Mungu amelikusudia laweza kutokea popote kwa sababu Mungu hana mipaka.

Akiamua kubariki anabariki, akiamua kuinua anainua, historia yako siyo kikwazo cha mafanikio yako. Mungu atakubariki tu acha waseme usiwasikilize, msikilize Mungu anayeongea nawe wakati huu ili akutukuze utakaa na wakuu wakati adui anakushangaa. Ubarikiwe sana na Bwana Yesu.

Mwalimu Frank Marino, anapatikana Usharika wa KKKT Ebeneza Nyashimo, Busega mkoani Simiyu. Maombi na ushauri tupigie kwenye simu 0783999044, 0786394705.