Kilo 500 za taka zaondolewa Mlima Kilimanjaro, wadau waonya

Moshi. Kampeni maalumu ya usafi iliyofanyika kwa siku tano katika hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro imefanikisha kuondolewa kwa zaidi ya kilo 500 za taka katika maeneo mbalimbali ya hifadhi hiyo, hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kulinda uhalisia na usalama wa kivutio hicho maarufu duniani.

Kampeni hiyo ilihusisha zaidi ya watu 43 wakiwemo wapagazi, waongoza watalii, wafanyakazi wa kampuni za utalii na wataalamu wa uhifadhi, ikiwa chini ya udhamini wa kampuni ya Zara Tours kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).

Kwa miaka ya karibuni, ongezeko la watalii na matumizi ya vifungashio vya bidhaa kumeongeza uchafuzi katika maeneo ya kupanda Mlima Kilimanjaro, hali inayowatia wasiwasi wadau wa utalii na wataalamu wa mazingira.

Mwenyekiti wa Chama cha Wapanda Mlima Tanzania (TAP), Ahmed Mkoma amesema kiwango cha taka kilichokusanywa kinaonyesha umuhimu wa kuongeza elimu na ukaguzi wa matumizi ya bidhaa ili kulinda mlima huo.

Baadhi ya takataka zilikuwa katika hifadhi ya taifa ya mlima Kilimanjaro



“Tulikuwa zaidi ya watu 43 na tumekusanya zaidi ya nusu tani ya takataka. Mlima ni ofisi yetu; hapa ndipo tunapoendesha maisha yetu. Uchafu ukiongezeka, usalama na afya ya watalii na wafanyakazi inatetereka,” amesema Mkoma.

Amesema taka nyingi zilizopatikana ni plastiki ndogondogo, mabaki ya chakula, vifungashio vya pipi na vinywaji pamoja na makopo yanayoachwa na wapandaji wa ndani na nje ya nchi.

“Tunawashukuru Zara kwa kutuwezesha kupanda mlima kufanya usafi. Tunaomba kampuni nyingine zijiunge nasi kwa sababu utalii hauwezi kunoga kama mazingira ni machafu,” ameongeza.

Amesema jumla ya kilo 530.5 za taka zilikusanywa, ingawa makadirio ya awali yalionesha zingeweza kufikia kilo 600 kutokana na maeneo mengine kuwa magumu kufikika.

Takwimu zinaonyesha kuwa kilo 48 zilikusanywa katika eneo la Shira 1 kupitia lango la Lemosho, kilo 128 kutoka Shira 1 hadi Shira 2 kupitia lango la Londorosi, huku kilo 172 zikipatikana Baranco, Karanga na High Camp (Millennium) kupitia lango la Mweka.

Mwongoza watalii kutoka Zara Tours, Gilbert Kasaba amesema uchafu mkubwa unatokana na vifungashio vya bidhaa za viwandani na masokoni.

“Tumekuta mabaki ya pipi, yoghurt, makopo ya vinywaji, vifungashio vya mikate na hata mabaki ya chakula. Tunataka wazalishaji wa ndani washirikiane nasi kwa sababu bidhaa zao ndizo zinazoleta mzigo mkubwa wa taka mlimani,” amesema Kasaba.

Ameeleza kuwa baada ya uchambuzi, watashirikiana na watengenezaji wa bidhaa hizo kwa kuwapa taarifa rasmi kuhusu hali ya mlima ili kuongeza ushiriki wao katika hatua inayofuata.

Mmoja wawa mdau wa utalii aliyeshiriki zoezi la siku tano la ukusanyaji taka Mlima Kilimanjarao aliwa na mifuko yenye taka walizokusanya



Mwalimu wa utalii na uhifadhi, Edfad Meshaki, amesema mabaki ya chakula yanaharibu tabia za wanyama waishio katika ukanda wa mlima.

“Ndege na nyani wanapokula mabaki kama mikate au ugali, mfumo wao wa kutafuta chakula unaharibika. Watalii wanapokuja wanataka kuona uhalisia, si wanyama waliozoea kula chakula cha binadamu,” amesema.

Meshaki ameongeza kuwa ni muhimu kulinda mlima huo kama urithi wa kizazi kilichopita na kijacho.

Afisa Rasilimali Watu na Utawala wa Zara Tours, Benard Gerard Saini, amesema kampuni yao itaendelea kushirikiana na Tanapa kuhakikisha mlima unabaki salama na vivutio vinabaki na ubora wake.

“Utalii endelevu hauwezekani bila usafi. Tunatoa rai utunzaji wa mazingira ufanyike muda wote, si kwa msimu mmoja,” amesema.

Askari Daraja la Pili Muikolojia wa Tanapa, Justine  Lazaro amesema zaidi ya kampuni 15 ziliungana mwaka huu kufanya usafi katika hifadhi hiyo.

“Kila ‘low season’ tunafanya shughuli hii. Mwaka huu tumefanikiwa sana, na makampuni zaidi ya 15 yamejitokeza, licha ya wengine kuanza kwa kuchelewa,” amesema.

Mmoja wa washiriki, Loveness Solomon amesema pamoja na kazi kuwa ngumu, wanawake wanajivunia kuwa sehemu ya juhudi hizo.

“Tulikuwa wanawake sita katika kundi la zaidi ya watu 35. Haikuwa rahisi, lakini tulipambana. Ni fahari kuonyesha wanawake wanaweza kulinda mlima wetu,” amesema.

Wadau wanasema kuongezeka kwa uchafuzi katika Mlima Kilimanjaro kunaweza kuathiri taswira yake kimataifa, kuharibu ekolojia ya viumbe na kupunguza thamani ya utalii unaoiingizia nchi mamilioni ya shilingi kila mwaka.

Kampeni nyingine inatarajiwa kufanyika mwakani, huku wadau zaidi wakihimizwa kushiriki kulinda mlima unaotajwa kama “nembo ya utalii Tanzania.”