KOCHA wa zamani Simba, Abdelhak Benchikha ameitahadharisha mapema Yanga kwamba ijiandae kukutana na ugumu katika mechi ya pili ya Kundi B dhidi ya wababe wa Algeria, JS Kabylie aliyowahi kuinoa kabla ya kuachana nayo mwaka huu, akisema jamaa ni wagumu mno.
Yanga imepangwa pamoja na vigogo wengine wa Afrika Kaskazini, Al Ahly ya Misri na AS FAR Rabat ya Morocco watakaovaana nao wikiendi hii katika mechi ya kwanza itakayopigwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Benchikha ambaye ni raia wa Algeria na aliyeondoka Msimbazi ghafla baada ya kuishuhudia Simba aliyokuwa akiinoa kunyukwa mabao 2-1 na Yanga, alisema ni kweli Yanga imepangwa kundi gumu lenye timu hizo tatu za Waarabu, lakini ina kazi nzito.
Benchikha aliyeipa USM Alger ya Algeria ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023 kwa kuitambia Yanga kwa kanuni ya bao la ugenini kutokana na mechi mbili za fainali baina yao kumalizika kwa sare ya 2-2, alisema licha ya Yanga kuwa wazoefu bado inapaswa kujihadhari.
Alisema licha ya timu hiyo kuwa na uzoefu na michuano ya kimataifa, lakini kumhofia mpinzani kunaweza kuwa ni mbinu nyingine ya ushindi kwao kwa sababu itawasaidia kujipanga mapema.
“Nitaitaja timu ninayoifahamu katika kundi walilopo, yaani JS Kabylie niliyowahi kuifundisha, kiukweli kwa sasa imebadilika baada ya kumaliza matatizo ya kifedha, imesajili wachezaji wazuri,” alisema Benchikha na kuongeza;
“Naiona Yanga kama imepepesuka kiubora na kama wanataka kufanya vizuri wanatakiwa kwanza kufanya vyema kwa mechi hiyo ya kwanza nyumbani ili wasiwe na presha kubwa itakapoenda ugenini kwa pambano la pili la kundi hilo. Changamoto kubwa ya mechi kubwa kama hizo ni kila timu inataka kufanya vizuri, kwa hiyo lazima kazi iwe ngumu kwa pande zote.”
Rekodi zinaonyesha JS Kabylie ya Algeria iliyomaliza ya pili msimu uliopita katika Ligi Kuu ya nchi hiyo nyuma ya MC Alger iliyotwaa ubingwa kwa tofauti na pointi mbili, imetinga makundi baada ya kuitupa nje US Monastir ya Tunisia, iliyowahi kupangwa kundi moja na Yanga katika mechi za Kombe la Shirikisho msimu ilipofika fainali dhidi ya USM Alger.
Kabylie ilishinda nje ndani dhidi ya Watunisia hao, lakini ikiwa na rekodi ya kuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa mara mbili 1981 na 1990 na kwa msimu huu katika Ligi ya kwao inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 15 kutokana na mechi tisa, huku ikipoteza mechi iliyopita kwa bao 1-0 mbele ya Constantine, ilihali Yanga inaongoza Ligi Kuu kwa pointi 1o kupitia mechi nne.
Katika kikosi cha JS Kabylie kuna staa mmoja kiungo Babacar Sarr ambaye misimu miwili iliyopita aliwahi kupita Simba kwa nusu msimu na sasa anang’aa ndani ya kikosi hicho.
Yanga itakutana na JS Kabylie Novemba 28 ugenini baada ya kumalizana kwanza na FAR Rabat ya Morocco wikiendi hii katika pambano la kwanza litakalopigwa kwenye Uwanja wa Amaan.