KAIMU Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC (CEO), Daniel Madenyeka, amesema licha ya mwenendo usioridhisha wa kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara, suala la kuachana na kocha wa timu hiyo, Mbrazil Marcio Maximo, bado halijafikia uamuzi wa mwisho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Madenyeka amesema hakuna kiongozi anayefurahishwa na mwenendo wa timu hiyo kwa sasa, ingawa hawawezi kufanya uamuzi wa mwisho kwa kocha huyo, hadi pale watakapoona ni muda na wakati sahihi kwao wa kufanya hilo.
“Maximo ni kocha wetu na bado ana mkataba, unapotaka kuuvunja ni lazima uupitie kwa umakini kujua ni mambo gani unapaswa kumlipa ili muachane salama, suala lake bado liko katika uongozi wa juu na likikamilika tutalitolea taarifa,” amesema.
Madenyeka aliyechukua nafasi ya Daniel Mwakasungula aliyeondoka, amesema katika uongozi wake hatakuwa tayari kuona timu hiyo inashuka daraja mikononi mwake, hivyo, watapambana zaidi kwa kushirikiana na wenzake ili kuinusuru.
Licha ya kauli ya Madenyeka, Mwanaspoti linatambua Maximo yupo katika hatua za mwisho za kuachana na kikosi hicho, ambapo kwa sasa kinachofanyika ni kuhakikisha kwanza wanamlipa fedha zake zote za kuuvunja mkataba ili ndio aondolewe.
Maximo tangu ajiunge na kikosi hicho msimu huu, ameshinda mechi moja tu ya Ligi Kuu, huku akichapwa tano mfululizo kati ya sita ilizocheza KMC, ambapo hadi sasa timu hiyo inaburuza mkia na pointi tatu, ikifunga mabao mawili na kuruhusu 10.
Hii ni mara ya tatu kwa Maximo kuja Tanzania kufundisha soka, baada ya awali kuifundisha Taifa Stars kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, kisha akaifundisha Yanga 2014, akiwa ni miongoni mwa makocha waliojizoelea umaarufu.
Maximo amerejea nchini akiwa na kumbukumbu nzuri, kwani ndiye kocha wa kwanza pia kuiongoza timu ya taifa ya Taifa Stars kufuzu ushiriki wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za ndani (CHAN), zilizofanyika huko nchini Ivory Coast mwaka 2009.