Mmesikia huko? Kapera ameanza tizi Polisi Tanzania

MSHAMBULIAJI wa maafande wa Polisi Tanzania, Ramadhan Kapera ameanza mazoezi ya kujiweka fiti na kikosi hicho, baada ya kukosekana tangu msimu huu umeanza, kutokana na kusumbuliwa na jeraha la goti alilolipata kutokana na kupata ajali ya gari.

Nyota huyo aliyewahi kuitumikia timu hiyo msimu wa 2020-2021, amerejea tena katika kikosi hicho msimu huu, baada ya kuachana na TMA ya jijini Arusha na kwa sasa ameanza mazoezi na muda wowote ataanza kucheza mechi za kiushindani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kapera amesema kwa sasa anajisikia vizuri baada ya kuanza mazoezi mepesi kutokana na majeraha ya goti na kifua aliyopata wakati wa ajali, hivyo, mashabiki wa kikosi hicho watarajie kumwona tena uwanjani.

“Kama mchezaji huwa inauma sana unapopitia kipindi kigumu cha namna hii usipocheza, kwangu nimeichukulia changamoto mpya ya kunipa nguvu zaidi nikirudi uwanjani, lengo letu kubwa ni kuipambania timu irudi tena Ligi Kuu Bara,” amesema Kapera.

Msimu wa 2024-2025, Kapera aliifungia TMA mabao sita ya Championship, akizichezea timu za Mbeya Kwanza, Geita Gold, KMC na Ihefu kwa sasa Singida Black Stars na anaipambania Polisi kurejea Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2022-2023.