MSHAMBULIAJI kinda wa Trident FC ya Zambia, Mourice Sichone amesema anataka kutafuta changamoto nje ya nchi hiyo baada ya kuitumikia ligi Daraja la Kwanza kwa takribani misimu miwili sasa.
Kinda huyo (18) alisajiliwa dirisha dogo akitokea Mpulungu Harbour FC ya nchini humo akicheza mechi 12 na kufunga mabao manne na asisti tano.
Akizungumza na Mwanaspoti kinda huyo amesema mbali na kukaa muda mrefu sababu nyingine ni ofa alizonazo kutoka Tanzania na nchi nyingine ingawa hakutaka kutaja jina.
Aliongeza kuwa, yuko nje ya uwanja kwa takribani miezi mitano akiuguza majeraha baada ya kuumia kidole mara mbili, na hivi karibuni alichezewa faulo kwenye enka itakayomuweka nje miezi miwili.
“Msimu huu haujawa mzuri kwangu nimeumia kidole mara mbili, nimepona naanza tu mechi ya kwanza ya kirafiki nikaumizwa tena kwenye enka. Daktari kasema jeraha sio kubwa, lakini naweza kukaa nje ya uwanja kwa miezi miwili,” amesema Sichone.
“Majeraha ni jambo gumu sana kwa wachezaji, naangalia msimu huu unaweza kuwa wa mwisho nirudi hata nyumbani niangalie timu ya kucheza ikishindikana basi hata zile za nje.”