Mradi wa Rostam wa gesi ya kupikia wapata kibali Kenya

Mombasa. Kampuni iliyoanzishwa na mfanyabiashara bilionea na mwekezaji wa viwanda kutoka Tanzania, Rostam Aziz, Taifa Gas Investments SEZ Ltd, imepata nafuu baada ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi (ELC) nchini Kenya kutupilia mbali kesi iliyopinga ujenzi wa kiwanda chake cha gesi ya kupikia (LPG).

Mradi huo wa kiwanda chenye thamani ya Dola 130 milioni za Marekani (takribani Sh320 bilioni) upo eneo maalumu la kiuchumi la Dongo Kundu, Likoni, Mombasa.

Mahakama imetupilia mbali ombi la wakazi wawili wa Likoni waliopinga ujenzi wa kiwanda hicho chenye uwezo wa kuhifadhi tani 30,000 za LPG, baada ya kukubali pingamizi la awali lililowasilishwa na Taifa Gas.

Akitoa hukumu, Jaji Stephen Kibunja amesema, leseni ya Tathmini ya Athari za Mazingira (EIA) Na. NEMA/EIA/PSL/21998 ilitolewa kihalali na idhini zote za kisheria zilizingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Uratibu (EMCA) ya mwaka 1999 pamoja na masharti ya kikatiba ya Kenya.

Akizungumza baada ya uamuzi kutolewa mwishoni mwa wiki, Rostam alisema kampuni yake imepokea hukumu ya shauri namba E006 la mwaka 2025 kama uthibitisho wa utii wa sheria na ulinzi wa mazingira.

“Huu ni ushindi unaothibitisha dhamira yetu ya kufuata utaratibu na kulinda mazingira. Pia ni hatua muhimu katika safari ya Kenya kuelekea kwenye nishati safi. Kituo chetu cha tani 30,000, ambacho ni kikubwa zaidi barani Afrika, kitapanua upatikanaji wa nishati safi, kuimarisha uthabiti wa nishati kikanda, na kufungua fursa mpya za ustawi,” alisema Rostam.

Alisema dhamira ya Taifa Gas katika kuleta maendeleo endelevu inavuka mipaka ya miundombinu.

“Mbali na kutoa suluhisho za nishati safi, tunajikita pia kuboresha maisha, hasa kwa wanawake wanaoishi katika maeneo yaliyo jirani na mradi. Kuwainua wanawake kiuchumi ni msingi wa kuhakikisha mradi huu unaleta matokeo yaliyojumuishi na ya kudumu.”

Katika hukumu, Mahakama imesema walalamikaji walikuwa sehemu ya jamii ya Likoni ambayo awali ilishawasilisha masuala hayo mbele ya NET mwaka 2022.

Kwa uamuzi huo, Mahakama imeweka kigezo muhimu cha kutoa hitimisho la migogoro ya mara kwa mara inayotokana na pingamizi kuhusu miradi iliyoidhinishwa kisheria.

Uamuzi huu unaimarisha imani katika mifumo ya usimamizi wa mazingira nchini Kenya na kuendeleza usawa kati ya haki za kimazingira na maendeleo endelevu.

“Tunashukuru kwa uwazi wa Mahakama, unaotuwezesha kuendelea mbele kwa kuzingatia utekelezaji ulio salama na endelevu,” alisema Dk Timothy Kyepa, Mshauri Mkuu wa Sheria wa Taifa Group na kuongeza:  

“Uamuzi huu unathibitisha kwamba, pale wawekezaji wanapofuata sheria na kulinda mazingira, taasisi za Kenya zitahakikisha usalama. Hili ni jambo jema kwa biashara, haki na maendeleo endelevu.”

Mradi huo unalenga kuimarisha usalama wa nishati nchini Kenya, kuhimiza matumizi ya nishati safi kwenye kaya na kutengeneza nafasi za ajira.

Vilevile, unaongeza ushindani na unafuu wa gharama za sekta ya nishati safi (LPG) ambao unaenda sambamba na Sera ya Nishati ya Taifa ya mwaka 2018.

Kwa mujibu wa mkakati wa Wizara ya Nishati nchini Kenya ya kuongeza matumizi ya LPG kutoka asilimia 24 hadi 70 ifikapo 2028, kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 30,000, kupunguza vikwazo vya uagizaji, kuleta utulivu wa bei na kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa uhakika wa nishati hiyo.

Pia, kitachochea ushirikiano wa kikanda kati ya Kenya na Tanzania, sambamba na malengo ya biashara ya kikanda chini ya mfumo wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na Umoja wa Afrika Mashariki (EAC).

Mradi huo ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa zaidi wa miundombinu ya LPG nchini Kenya, ukiwa na lengo la kupunguza gharama za nishati, kuimarisha usalama wa nishati na kutoa ajira.