Ripoti ya mwaka 2017 iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ustawi wa Watoto (Unicef), ilibainisha kuwa mtoto anayeishi kwenye maeneo yenye matukio ya vurugu kama mapigano, milipuko ya mabomu au mauaji hupata madhara kadhaa ya kisaikolojia.
Hata katika mazingira ambayo mtoto si mlengwa wa moja kwa moja na matukio hayo, ile kushuhudia damu, milio ya risasi, au mtu mwingine akiumizwa mbele yake huacha alama inayoweza kumsumbua kwa muda mrefu.
Katika maeneo yanayoathirika zaidi na matukio haya ni hisia. Bruce Perry na Bessel van der Kolk, ambao kwa miaka mingi wametafiti namna hisia za mwanadamu zinavyoweza kuathirika na kuacha makovu yenye nguvu ya kuharibu ustawi wa mtu wanaweza kutusaidia kuelewa.
Kwa kawaida, matukio haya huzua taharuki kwa mtu, hali inayoweza kujenga hofu kubwa kwa mtoto. Amygdala, yaani sehemu ya ubongo inayosimamia hisia za hofu, ikichochewa na hali ya tishio, mtoto hupata mshtuko unaozalisha kemikali za kujilinda na tishio hilo.
Ingawa uzalishaji huu wa homoni una umuhimu wake kwa binadamu, inakuwa kwa mtoto mdogo, mfumo huu hauna uwezo wa kurejea katika utulivu kwa urahisi kama inavyokuwa kwa mtu mzima, jambo linalomfanya abaki katika hali ya taharuki hata baada ya tukio kupita kwa muda mrefu.
Matukio ya vurugu hubeba maumivu ambayo si rahisi kuyaona. Tunaweza kumwona mtoto kama “ametulia” na anaendelea na michezo yake kama kawaida lakini ndani yake akawa amebeba picha zinazojirudia mara kwa mara kichwani na hivyo kumnyima utulivu wake wa kawaida.
Hali kama hiyo inaweza kumfanya mtoto awe na usingizi wa shida, alie bila sababu, aogope sauti zinazofanana na milio alioisikia, au kuogopa kuwa mbali na mzazi wake.
Wengine hurudia zile tabia za kitotototo kama kukojoa kitandani, kupoteza hamu ya kucheza, au hupandwa hasira zisizo na maelezo. Watoto kama hawa mara nyingi hutafsiriwa vibaya kuwa wakorofi au wabishi, ilhali kinachoendelea ni mwitikio wa mwili na akili baada ya hofu kali.
Pia, hofu ya muda mrefu huathiri sehemu za ubongo zinazohusika na ujifunzaji na matokeo yake ni kudhoofisha uwezo wa kukumbuka. Hii ndiyo maana mtoto aliyewahi kushuhudia tukio la kutisha anaweza kushuka kitaaluma au kupoteza umakini anapokuwa darasani.
Nguvu ya utulivu wa mzazi
Kuna dhana muhimu katika saikolojia ya watoto inayoitwa co-regulation yaani uwezo wa mtu mzima kutumia utulivu wake kumsaidia mtoto kurudia hali ya kawaida. Mzazi au mlezi akiwa mtulivu, mwenye huruma na anayesikiliza, husaidia ubongo wa mtoto kutulia na kujenga hisia za usalama.
Mzazi anapomkemea mtoto kwa kuogopa au kulia, anaongeza hofu badala ya kuipunguza. Kauli rahisi kama “Najua umeogopa, lakini sasa tuko salama” inaweza kuwa tiba tosha ya kihisia. Kukaa karibu, kumkumbatia au kumshika mkono ni njia ambazo tafiti zimeonyesha kuwa huongeza utolewaji wa homoni ya upendo (oxytocin), inayosaidia kupunguza msongo wa mawazo.
Ni muhimu pia kuepuka kumwambia mtoto “sahau” au “kuwa jasiri.” Badala yake, mpe nafasi ya kueleza alichokiona au kukielezea kwa njia anayoimudu kupitia mchoro, mchezo au mazungumzo mafupi.
Kumrudisha kwenye hali ya kawaida
Baada ya mtoto kushuhudia tukio la kutisha, hatua kubwa ya uponyaji ni kumrudisha katika hali ya maisha ya kawaida. Hii inaweza kuwa kwa kurudi shule, kucheza na wenzake, au kushiriki shughuli za familia kama kawaida. Utaratibu wa kila siku humsaidia ubongo wake kuelewa kwamba dunia haijafikia mwisho. Ile kuona maisha yanaendelea kama kawaida huondoa picha za hofu taratibu.
Mzazi anaweza kusaidia kwa kuweka utulivu wa mazingira ya nyumbani, kuepuka mijadala ya mara kwa mara kuhusu tukio ambalo mtoto alilishuhudia, na kuhakikisha mtoto analala na kula vizuri.
Lakini pale dalili zinapoendelea kama mtoto kuota ndoto mbaya mara kwa mara usiku, kutozungumza kabisa, au kuwa na hasira zisizoelezeka kwa muda mrefu, ni muhimu kumshirikisha mtaalamu wa saikolojia ya watoto.
Watoto wanaoshuhudia matukio yanayoumiza hisia hubeba majeraha yasiyoonekana kwa macho, lakini yanayoweza kudumu kwa muda mrefu na wakati mwingine maisha yote.
Mzazi au mlezi akiwa na uelewa mzuri anaweza kuwa tiba muhimu kwa hisia za mtoto kuliko hata dawa anayoweza kupewa mtoto. Upendo, uvumilivu na utulivu wa mzazi humfanya mtoto ahisi yuko salama tena.
Tukumbuke, uponyaji kwa mtoto huanza na kujihisi yuko salama. Mchakato wa uponyaji huo huanza pale mtoto anapojisikia kuwa yupo karibu na mtu anayemhakikishia kuwa yupo kwenye mikono salama.