Penzi la mitego linavyowaliza wanawake kiuchumi

Dar es Salaam. Hali ikiwa ya utulivu, kila mmoja akiendelea na lake ndani ya saluni ya kike iliyopo Mwenge, msichana mwenye umri wa miaka 26 anapaza sauti inayoashiria kukata tamaa.

“Natafuta mganga mzuri ambaye anaweza kunisaidia… nina janga, sielewi nalitatua vipi.”

Ni kauli iliyotoka kwa mtu aliyelemewa mzigo wa deni ndani ya kikundi cha kuweka na kukopa (kikoba), lililotokana na mtu aliyemtapeli.

Katika miezi minne ya uhusiano aliyodhani ungekuwa mwanzo mpya, ndipo alipoangukia kwenye mtego wa mtu aliyemvuta kwa maneno matamu na matumaini ya kufunga ndoa, kisha akakomba fedha na kutoweka kama kivuli cha jioni.

Kisa cha msusi huyo (jina linahifadhiwa) si cha kwanza. Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na simulizi kadhaa za matukio kama lililomfika.

Wapo wanawake wanaoingia kwenye uhusiano kwa imani kuwa wamepata wenza wa maisha, badala yake hujikuta wakipoteza fedha, wakiumizwa kisaikolojia na kuingia kwenye mzigo wa madeni.

Miongoni mwa walioathirika ni wanawake wafanyakazi wa saluni wanaojituma kutafuta riziki ya halali, wakiwa na uhakika wa kipato cha kila siku.

Walimu wanaoheshimika, wanaoaminika na jamii, nao wamenaswa kwenye mtego huu wa ahadi tamu za kimapenzi.

Simulizi za wanawake watatu wa saluni na walimu wawili zinafanana kama kwamba ni tukio moja.

Wanaume wenye maneno matamu, magari ya kuazima, ahadi za biashara na ndoa wamekuwa wakichukua fedha kwa ahadi ya ama kurudisha au kushiriki miradi, kisha kutoweka ghafla wakiacha majeraha ya moyo na mizigo ya madeni.

Akizungumza na Mwananchi akiwa saluni, msusi huyo anasema kutokana na bidii yake ya kazi, alifungua saluni yake eneo la Mabibo Hostel.

Akiwa hapo anasema alikutana na kijana aliyejitambulisha kwa jina moja la Moris. Alikuwa na gari, mtanashati na alionekana mwenye uwezo wa kifedha.

Katika muda mfupi, walijenga uhusiano. Anasema Moris alikuwa akimtembelea ofisini kwake kila saa moja jioni.

“Yule kaka huwezi kufikiri ni tapeli. Nilikutana naye wakati nasubiri daladala ya kuelekea Simu2000 maarufu Mawasiliano, alinipa lifti. Tukiwa ndani ya gari alinisifu, akieleza nafaa kuwa mke wa mtu. Aliniambia haya baada ya kuniuliza iwapo nimeolewa,” anasema.

Anasema alinasa kwenye ulimbo, wakabadilishana namba za simu. Badala ya kumshusha kituo cha daladala, alimpeleka hadi nyumbani kwake Sinza Vatican.

Simu za mara kwa mara zikachipusha penzi kati yao. Ilikuwa ni zaidi ya dozi ya dawa ya kutwa mara tatu, kwani Moris alimpigia simu hata mara nne, akimjulia hali na kutaka kufahamu mwenendo wa kazi, akionesha kujali.

“Usiku sikulala vizuri, alikuwa akitaka muda mwingi tuzungumze, akinisifia kwa hiki na kile. Sikutambua ana lake jambo moyoni, kila nikikumbuka nalia sana,” anasema.

Ndani ya miezi mitatu anasema alimweleza mambo mengi Moris, aliyejitambulisha kwake kuwa ni mtumishi wa Serikali.

Katikati ya wiki alikuwa akivaa nadhifu kama mtu aendaye ofisini, isipokuwa mwisho wa juma alikuwa akivaa fulana na suruali ya jeans.

Kutokana na mwonekano wake na zawadi za bidhaa za saluni alizokuwa akimpelekea, anasema ilikuwa ngumu kubaini kuwa ni tapeli.

Mahaba yalipokolea, kuna wakati walikwenda wote Kariakoo, ambako alimnunulia mahitaji ya saluni.

Katika kumhakikishia kuwa hakuwa na nia mbaya, alimuonesha baadhi ya alioeleza kuwa ni ndugu zake.

“Nilimuamini mno. Kuna siku alikuja na wageni, akanitambulisha kuwa ni ndugu zake. Alikuwa binti mmoja na kina kaka wawili. Nilikaa nao kama dakika 20, wakaondoka kwa ahadi ya kurudi tena kunitembelea,” anasema.

Hata hivyo, hakuwahi kumpeleka nyumbani kwake, akimweleza muda mwingi anautumia kazini.

Kwa upande wake, msusi huyo anasema mwishoni mwa juma huwa ana kazi nyingi, hivyo haikuwa rahisi kwake kuacha biashara na kwenda kumtembelea Moris.

“Julai tuliongea vitu vingi kuhusu maisha, na siku hiyo nilimwambia sina pesa, nadaiwa kikoba. Nilikuwa nahitaji Sh1 milioni kwa ajili ya kulipa deni, nikope tena,” anasema.

Anasimulia kuwa Moris alimwambia ni jambo dogo, hivyo angempatia siku inayofuata ili kulipa pesa hizo. Kweli alipelekewa fedha hizo kama alivyoomba, akielezwa kwa shida ndogo hana sababu ya kukopa kutoka kikoba.

“Baada ya kulipa deni kikoba, siku ya nne aliniambia gari lake limepata tatizo la injini, anahitaji Sh6 milioni ambazo angelipa ndani ya siku tatu,” anasema.

Msusi huyo anasema alikwenda kikoba, akakopa kiasi hicho cha fedha, akampatia.

Kwa kitendo hicho ni kama alijipalia makaa. Anasema simu ya Moris haikupatikana tena, akatoweka machoni na masikioni mwake, akimwachia mzigo wa deni la kulipa kikoba.

Kwa upande wake, Astridah Macha, mkazi wa Mbande, anasema alipokutana na Kelvin, kijana msomi, aliamini ameachana na maisha ya kuwa single.

“Nataka tuanze maisha mapya, nataka kukuoa,” Kelvin alimwambia mara kwa mara, hivyo alijinasibu kuwa ana mume mtarajiwa.

Siku ziliposonga, Kelvin alianza kumweleza changamoto za kifedha zinazomkabili akitaka msaada.

Astridah, akimwamini mpenzi wake huyo, alikopa Sh500,000 kutoka kikoba, akachanganya na fedha zake nyingine, akamkabidhi Sh1 milioni.

Anasema akiwa ameanza kurejesha mkopo, Kelvin alitoweka maishani mwake.

Katika kundi hilo la wasusi, yupo pia Rehema Mtumbuka, mkazi wa Kurasini, aliyekuwa na ndoto ya kuwa mke wa Dullah, aliyekuwa akimtembelea kwa usafiri wa pikipiki.

“Uwe na uhakika mimi ndiye mwanamume wako wa maisha,” Dullah alimuahidi kabla ya kumpiga mzinga wa kusaidiwa mtaji wa biashara ya vifaa vya umeme.

Akiamini anamsaidia mume mtarajiwa, Rehema alikopa Sh700,000 kwa jina lake, kisha akaongeza na Sh300,000, hivyo akamkabidhi Sh1 milioni.

Kufumba na kufumbua, Dullah akawa ametoweka. Alipofuatilia kwa marafiki zake alielezwa pikipiki aliyokuwa akisafiria ni ya kuazima.

Husna Mwinyi, mwalimu wa shule ya msingi iliyopo wilayani Kinondoni, anasema aliolewa na Seif Pazi, mjasiriamali wa biashara ya vifaa vya ujenzi.

Anasema waliishi miaka miwili kwa amani, hadi alipomshawishi achukue mkopo wa Sh15 milioni ili abadili biashara kwa kuanzisha ya usafirishaji wa mbao.

Akiamini ni hatua ya kuboresha maisha yao, Husna anasema aliomba mkopo, lakini miezi miwili baada ya kupokea fedha, Pazi alitoweka.

Alipofuatilia, anasema alibaini Pazi ameoa mwanamke mwingine Kigamboni na amemuachia mzigo wa deni na malezi ya mtoto mmoja waliyempata katika ndoa yao.

Lucia Singano, mwalimu wa sekondari wilayani Temeke, anasema alikutana na Masoud Mohamed kwenye semina ya walimu iliyofanyika Dodoma.

Anasema alionekana mtu mwadilifu na mwenye maono, na walipoanza uhusiano wakiwa na dhamira ya kujenga maisha pamoja.

Anasema uhusiano wao ulikomaa ndani ya muda mfupi, akimuamini mtumishi mwenzake wa Serikali.

“Sijui ilikuaje, ni kama alinipa dawa. Kwa muda mchache nilimuamini, nikajikuta nampenda zaidi, na kila alichokuwa ananiomba nilimpatia, hata kama sina, nakopa kwa ajili yake,” anasema.

Anasema alikuwa akimlilia shida za kifedha, ikiwamo kodi, na alimuachia kadi yake ya benki endapo mshahara ukingia akatoe pesa anazomdai.

“Nilimpatia Sh3 milioni, maana kila siku alikuwa anakuja na jambo jipya. Mwisho wa mwezi nilikwenda kutoa pesa kutumia kadi yake, namba ya siri iligoma. Walimu wenzangu wakaniambia itakuwa amebadilisha kadi,” anasema.

Baada ya uchunguzi, anasema alibaini Masoud ana mke na watoto wawili.

Alipomuuliza kuhusu fedha zake, alimjibu: “Nimeamua kurudi nyumbani, samahani kama nimekuumiza.”

Mwanasaikolojia Clara Mwambungu anasema aina hii ya udanganyifu hutokea zaidi kwa wanawake wanaotafuta uthabiti wa kihisia na usalama wa maisha.

“Wanaume hawa hutumia mbinu za emotional manipulation (udanganyifu wa kihisia), maneno matamu, ahadi za ndoa na matumizi ya hadhi ya uongo kama magari ya kuazima. Wanawake hujenga imani haraka pale wanapoamini wamepata mwenzi anayejali,” anasema.

Anasema baadhi ya wanawake wanaopitia msukumo wa kijamii kuhusu ndoa na maisha bora hujikuta wakifanya uamuzi bila kujiridhisha.

“Wanawake hawa hawana tatizo la udhaifu, wanachokosa ni ulinzi wa kisaikolojia na ujuzi wa kutambua tabia za kitabaka zinazotumiwa na matapeli wa mapenzi,” anasema.

Mtaalamu wa fedha, Thomas Mrope, anasema wanawake wengi wanaingia kwenye madeni kwa sababu wanachanganya mapenzi na uamuzi wa kifedha bila utaratibu.

“Fedha ni jambo la hatari zaidi kuliko mapenzi. Ukichanganya vyote bila mikataba, ushahidi au mipaka ya uwajibikaji, unajipeleka kwenye hatari ya kupoteza kila kitu,” anasema.

Anasema si sahihi kumkopesha mtu fedha kwa sababu tu mna uhusiano.

“Ukiona mtu anakutaka ili umpe pesa, hayo si mahusiano, ni biashara ya ujanja. Hakuna mpenzi wa kweli anayekimbiza mwenza wake kuingia kwenye mikopo mikubwa,” anasema.