Dar es Salaam. Maisha uliyopitia yanaweza kujenga wazo linaloweza kukutambulisha duniani.
Ndivyo ilivyo kwa Gibson Kawango, ambaye awali alitaka kuwezesha familia yake kupata nishati ya umeme, sasa anatambulika kimataifa na wengi wananufaika na ubunifu wake.
Utambuzi huo ni kutokana na kuwezesha upatikanaji wa nishati ya umeme kwa kutumia betri mbovu za kompyuta mpakato kutengeneza mfumo unaoweza kuchajiwa kwa jua. Kwa sasa baadhi ya familia za vijijini zinanufaika.
Mradi huo sasa unawezesha kufunga vituo vya kuchaji magari ya umeme majumbani, kwenye maeneo ya umma nchini Tanzania.
Kupitia ubunifu huu, Kawago amepewa tuzo ya Kimataifa ya Kibinadamu ya Muhammad Ali (Muhammad Ali Humanitarian Award) katika kipengele cha ‘Giving’ kwa kazi anayofanya kupitia miradi ya Waga.
Akizungumza na Mwananchi, Kawago anasema tuzo hiyo hupatikana kwa kupendekezwa.
“Nilipopendekezwa jopo la majaji lilipitia kazi zangu na kuona matokeo makubwa tuliyofanya katika jamii,” amesema.
Kawago ni Mtanzania wa kwanza kushinda tuzo hiyo ya kimataifa. Kituo cha Muhammad Ali kimewajumuisha washindi kwenye mpango wa mwaka 2026, hivyo Tanzania ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimataifa wa kibinadamu.
Tuzo hiyo hutambua watu wanaoendeleza maadili mema, bidii, kujitoa, heshima na kuwa na roho nzuri kupitia kazi zao za kijamii kwa kuangalia manufaa yake na kuangalia zitakuwa na mchango gani kwa siku za baadaye.
Katika hafla ya mwaka huu, Mtanzania huyo ni miongoni mwa washindi 10 katika vipengele tofauti.
Kawago mzaliwa wa mkoani Iringa, ambaye ni mhitimu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) katika fani ya uhandisi wa umeme amesema wazo alilipata akiwa nyumbani kwao, wakati ambao familia zililazimika kutumia mbinu za ziada kuchaji simu zao.
Mbali ya vifaa vya kutunza chaji, pia huzalisha betri zenye uwezo wa kuwasha vifaa vingine vinavyohitaji nishati ya umeme kama runinga, hivyo kuwezesha baadhi ya nyumba kuondokana na matumizi ya vibatari.
Amesema kutokana na kukosekana nishati ya umeme kijijini kwao, watu walilazimika kutumia muda mrefu kufuata ilipo nishati hiyo ili kuchaji simu zao za mkononi.
Kwa wakati huo akiwa shule ya msingi alipenda kutengeneza redio na simu za watu, ndipo wazo la kutafuta namna ya kuchaji simu lilipomjia na akaamua kujaribu.
“Kwa wakati ule niliamua kutengeneza power bank kwa kutumia betri lakini haikuwa na uwezo wa kuchaji simu hadi ijae, niliamua kuendelea kutafuta ufanisi zaidi,” anasema.
Anaeleza udadisi uliongezeka kwa kadri alivyosonga mbele kielimu.
Alipofika chuo jijini Dar es Salaam alihisi betri za laptop zinaweza kufanya kazi kwa ufanisi ndipo alipoziokota kwenye masoko ya Kariakoo na Machinga Complex, akazivunja ili kuzitafiti.
Baadaye aligundua iwapo zitafanyiwa urejeleshaji zinaweza kuwa power bank yenye nguvu.
“Nikawa kila nikitengeneza najaribu na marafiki zangu, nyingine zilikubali, nyingine zilikataa. Nilipomaliza chuo niligundua namna ya kutengeneza kwa kutumia kompyuta na aina tofauti za saketi,” anasema.
Likiwa ni wazo lililodumu kwa zaidi ya miaka 12 sasa tangu aanze kulifanyia kazi, aligundua kupita betri hizo anaweza kutengeneza kubwa zenye uwezo wa kutumika nyumbani, zikiwa na uwezo wa kuwasha taa, kuangalia runinga, kusikiliza redio na kuchaji simu.
Betri hizo hupatikana kwa kuunganisha pamoja betri za laptop na kupata moja kubwa inayounganishwa kwenye inverter. Betri hizo huweza kuchajiwa kwa umeme jua na baadaye mtu akatumia umeme katika kuwasha vifaa tofauti ndani ya nyumba. Vijiji kadhaa nchini vimenufaika na huduma hiyo. Wanufaika wengine ni wamiliki wa pikipiki za umeme za kuchaji.
Kawago amekuwa akiwasaidia kuwabadilishia betri baada ya zile za awali kwisha nguvu au kufa.