Mbeya. Wakati msimu wa kilimo kwa mwaka 2025/26 ukianza, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Nyanda za Juu Kusini imekuja na teknolojia mpya na ya kisasa kukabiliana na magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao ili kumsaidia mkulima kuvuna kwa tija.
Teknolojia hiyo aina ya ‘Portable DNA Sequencing’ inayotajwa kuwa mwarobaini wa kukabiliana na magonjwa shambani na visumbufu mimea, imeanza na hatua za kuandaa shamba hadi kuvuna.
Ujio wa teknolojia hiyo huenda ikamaliza kilio cha baadhi ya wakulima hasa mpunga na kahawa waliokuwa wakikabiliwa na wadudu, magonjwa na vusumbufu mimea kuondokana na adha hiyo.
Mapema mwaka huu 2025 wakulima wa mpunga wilayani Mbarali walivamiwa na ndege aina ya kwereakwerea, huku upande wa kahawa huko wilayani Mbozi mkoani Songwe wakikabiliwa na wadudu aina ya konokono walioathiri mazao hayo kwa kushusha kiwango cha uzalishaji.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Novemba 16, 2025, meneja wa mamlaka hiyo, Pius Kawala amesema tayari teknolojia hiyo imeanza kutumika na kuleta matokeo mazuri katika baadhi ya mazao na mbogamboga ikiwamo vitunguu, nyanya na viazi.
Amesema awali matumizi ya maabara yalikuwa yakichelewesha matokeo hadi kufikia wiki moja, lakini kwa teknlojia hiyo inaenda kuwa mwarobaini kuondoa changamoto za mimea kwa wakulima.
Muonekano wa mimea ya kahawa iliyoshambuliwa na wadudu aina ya konokono katika moja ya shamba wilayani Mbozi mkoani Songwe
“Tayari imeundwa timu inayozunguka kwa wakulima ‘maabara shambani’ lengo ni kuangalia aina ya visumbufu kuanzia hatua ya maandalizi ya shamba hadi kuvuna, hii teknlojia ndio mwarobaini,” amesema.
“Matarajio yetu tuwape matumaini wakulima kuwa hatua hii inaenda kuwaondolea changamoto ya visumbufu vya namna yoyote shambani na watalima na kuvuna kwa tija, mamalaka imejipanga vyema,” amesema Kawala.
Meneja huyo ameongeza ili kufikia malengo ya Serikali kuwahudumia wananchi, wakulima wanaombwa kutoa ushirikiano na taarifa wanapoona uwapo wa dalili zozote za uwapo wa magonjwa, wadudu au visumbufu mimea.
Baadhi ya wakulima wamesema bado teknolojia hiyo haijawafikia wakiomba Serikali na mamlaka hiyo kuwafikia, wakieleza kuwa visumbufu mimea imekuwa changamoto kwao.
Hamphrey John, mkazi wa Utengule Usongwe wilayani Mbeya amesema wakulima wa viazi wanasubiri teknolojia hiyo inayoweza kuwasaidia kuvuna kulingana na kiwango chao.
“Kuna wakati tunavuna tofauti na uwekezaji wenyewe kutokana na changamoto ya magonjwa na wadudu kushambulia mazao, tupongeze kwa ubunifu huo ambao kimsingi utatusaidia kufikia malengo,” amesema John.