Njombe. Jamii ya Watanzania imeshauriwa kumrudia Mungu kwa kuhakikisha inatenda mambo mema na kuhubiri haki ili kutunza na kuilinda amani iliyopo hapa nchini.
Ushauri huo umetolewa leo Novemba 16, 2025 na Mwinjilisti wa Kanisa la Waadventisti Wasabato, Mkoa wa Njombe, Andrew Chikwanda wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Njombe.
Mwinjilisti huyo ameyasema hayo zikiwa zimepita siku 18 tangu ulipofanyika uchaguzi mkuu uliotawaliwa na maandamano yaliyozua vurugu zilizosababisha vifo, uharibifu wa mali za umma na binafsi.
Amesema ukaidi wa kuzitekeleza amri 10 za Mungu kwa wanadamu umesababisha madhila yanayotokana na nguvu ya shetani inayopandikizwa kwa watu.
Amesema vitendo vinavyofanywa na wanadamu hivi sasa ni chukizo machoni mwa Mungu, hivyo kila mmoja anapaswa kumrudia kwa kutenda mema na kuhubiri haki.
Amesema kwa kufuata na kutekeleza amri za Mungu, jamii itatenda haki na kuvumiliana katika masuala mbalimbali hivyo na amani itaendelea kuwepo nchini.
“Hapo zamani familia zilikuwa zinajua kuwalea watoto wao ili wawe na heshima kwa watu wanaowazunguka na neno la mungu linawajenga vijana na watoto kuwaheshimu binadamu wenzao,” amesema Chikwanda.
Amesema matukio mengi mabaya yanayotokea katika maeneo mbalimbali duniani ni kwa sababu ya watu kumsahau Mungu na kutenda mambo maovu yasiyompendeza mungu.
Kwa upande wake, Mwinjilisti Joseph Mungale wa Kanisa la Wadventisti Wasabato amesema vijana wakimfuta mungu kwa kutii neno lake wataweza kuepukana na changamoto ambazo zinawakabili.
“Vijana wanatakiwa kutii upande wa Serikali lakini pia upande wa Mungu kwani ukiharibu upande mmoja lazima na mwingine uharibu,” amesema Mungale.
Mkazi wa Njombe, Christina Mange amesema vijana wana nafasi kubwa ya kubadilisha taifa endapo watafuata neno la mungu na kuishi kwa kufuata maadili mema.
“Tunaishi katika ulimwengu ambao umechanganyikiwa hivyohivyo tuishi katika maelekezo ya mungu kwani tuna nafasi ya kuliandaa na kulisaidia taifa katika changamoto nyingi linalopitia,” amesema Mange.