YANGA imebakiza siku mbili tu za kulala jijini Dar es Salaam na baada ya hapo itatua Zanzibar tayari kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya kukutana na FAR Rabat ya Morocco katika mchezo wa kwanza wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Lakini, hivi unaposoma hapa elewa kwamba wababe hao wa Ligi Kuu Bara wanaendelea kupambana chini kwa chini na tayari wamewanyoosha wapinzani wao nje ya uwanja huko Zanzibar.
Kama ambavyo Mwanaspoti lilikuhabarisha jana kwamba Yanga itaondoka Dar Jumanne hii ya Novemba 18, 2025 ikienda Zenji kuwa mwenyeji wa FAR Rabat kwenye mchezo huo utakaopigwa Novemba 22 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, lakini imefanikiwa kushinda ‘vita’ ya kwanza dhidi ya Waarabu hao kwa kuwapiga bao kwenye ishu ya hoteli waliyokuwa wakiitaka pia.
Ikumbukwe kuwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wanacheza mchezo wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika wa kundi B.
Wakati siku zikiwa zinahesabika mabosi wa Yanga wameipiku FAR Rabat ambapo wote walijikuta wakitaka kufikishia vikosi vyao katika hoteli ya kitalii moja inayoitwa Madinat, lakini mabosi wa Jangwani wakawawahi wenzao na hapo ndipo kikosi chao kitakapofikia.
Katika hesabu zake Yanga inaamini kutumia hoteli hiyo itakuwa ni bahati kwao, kwani imewahi kufikia hapo na kwenda kushinda kwa kishindo kwenye mechi ya michuano ya CAF.
Msimu uliopita Yanga iliitumia hoteli hiyo kisha ikaenda kushinda kwa mabao 6-0 dhidi ya CBE ya Ethiopia na kutinga hatua ya makundi kibabe.
Mchezo huo ulikuwa na presha kubwa ambapo Yanga ilitoka kushinda ugenini kwa bao 1-0, huku ikionekana kama ilicheza chini ya kiwango, lakini ikiwa katika hoteli hiyo mechi ya hapa nyumbani ikawafurahisha mashabiki wake.
Mbali na mchezo huo Yanga imewahi kutokea hapo kisha kwenda kubeba ubingwa wa Kombe la Mapinduzi Zanzibar kwa matuta dhidi ya Simba kwenye mchezo wa fainali 2021.
Mmoja wa viongozi wa Yanga ameliambia Mwanaspoti kuwa, “tumeshaichukua hoteli na timu itafikia hapo kuanzia Jumapili (yaani leo). Watu wetu wataondoka hapa (Dar) kutangulia ili kuhakikisha maandalizi ya kupokea timu yanakuwa sawasawa.
“Watu wanaona ni ngumu, lakini sisi tunafurahia hilo (la kuwahi hoteli) kwani linatupa umakini kwamba, tunatakiwa kuwathibitishia tutafanya vizuri kwenye mechi hiyo.”
Hatua ya Yanga kuichukua hoteli hiyo itaifanya FAR Rabat kuangukia hoteli nyingine (jina tunalo), ambayo ilitumiwa na wenzao wa RS Berkane wakati wakicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Simba msimu uliopita ambapo walitoka sare ya bao 1-1 na kuchukua ubingwa