Clara ajipanga kuvunja rekodi yake Saudia

NYOTA wa Kitanzania, Clara Luvanga amesema anapambana kuhakikisha kila msimu anavunja rekodi zake mwenyewe za misimu iliyopita.

Hadi sasa, Clara anaongoza kwenye mbio za ufungaji bora ikiwa ni raundi ya sita ya Ligi Kuu ya Wanawake Saudia akiweka kambani mabao 11 na asisti tatu.

Akizungumza na Nje ya Bongo, Clara amesema kwake ni faraja kuona kila msimu anaendeleza ubora wake licha ya upinzani mkubwa anaokutana nao kwenye ligi hiyo ya pesa.

“Rekodi huwa naziweka ili nizivunje mwenyewe, nashukuru Mungu hadi sasa kuonyesha kiwango kizuri na kama nitaendelea hivi basi unaweza kuwa msimu wa bahati kwangu na malengo ni kuendelea kukaa nafasi hiyo hiyo ya kwanza,” amesema Clara.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga Princess na Dux Lugrono ya Hispania, amefikia rekodi ya msimu wake wa kwanza kucheza Saudia alipofunga mabao 11 na asisti saba za ligi.

Msimu uliopita ambao ulikuwa wa pili kwake aliivunja rekodi hiyo na kufikisha idadi ya mabao 21 na asisti saba zilizoipa timu hiyo ubingwa wa tatu mfululizo.

Kwa mabao 11 kwenye mechi sita, ana wastani wa kufunga mabao mawili kwa kila mechi.