Mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baina ya Yanga na Simba ‘Kariakoo Derby’ iliyokuwa ichezwe Desemba 13 mwaka huu, sasa itachezwa Machi Mosi, mwakani.
Hiyo inafuatia maboresho ya ratiba ya Ligi Kuu yaliyotangazwa leo na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Kubadilishwa kwa ratiba ya mchezo huo, kunafanya mwezi Machi mwakani, kunafanya timu hizo kukutana ndani ya muda wa miezi miwili tu katika Ligi Kuu kwani mchezo wa marudiano baina yao umepangwa kuchezwa Mei 3, 2025.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo ya ratiba, mchezo ulioahirishwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya TRA United na Simba ambao awali ulipangwa kufanyika Oktoba 30, sasa utafanyika Desemba 3, mwaka huu.
Mchezo baina ya Singida Black Stars ambao nao ulipangwa kufanyika Oktoba 30 sasa utafanyika Desemba 3 huku ule wa Tanzania Prisons dhidi ya Yanga ukipelekwa hadi Desemba 2, mwaka huu.
Maboresho hayo ya ratiba yameonesha kuwa msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2025/2026 utafikia tamati Mei 29, 2026 kwa mechi za raundi ya 30.
Ligi hiyo inatarajiwa kusimama kwa siku 46 kupisha Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Morocco kuanzia Desemba 21 mwaka huu hadi Januari 18 mwakani.
Katika hatua nyingine, Hafla ya Tuzo za Ligi Kuu 2024/2025 zimepangwa kufanyika Desemba 5, 2025.