Dakika 540 za Msuva Iraq

WINGA wa Kitanzania, Simon Msuva hajaanza vyema Ligi Kuu Iraq akiwa na kikosi cha Al Talaba SC baada ya kucheza dakika 540 na kufunga bao moja.

Ni msimu wa pili kwa winga huyo wa zamani wa Wydad AC ya Morocco na Yanga, kuitumikia Talaba, ambako msimu uliopita alifunga mabao 12 kwenye mechi 11.

Msimu huu tayari amecheza mechi sita akifunga bao moja dhidi ya Duhok Oktoba 3, bao lililoipa ushindi wa mabao 2-1 timu hiyo.

Kwenye mechi zote sita alicheza dakika 90 dhidi ya Zakho wakishinda bao 1-0, Al Zawraa 1-1, Al Naft wakipoteza kwa mabao 3-0, Al Najaf wakipoteza bao 1-0 na Naft Missan wakiondoka na ushindi wa mabao 2-1.

Hata hivyo, tangu hapo Msuva hajafunga bao lolote licha ya takwimu zikionyesha kwenye mechi sita alizocheza msimu uliopita alikuwa tayari ameweka kambani mabao matatu.

Hali hiyo pia inaonekana kuwa changamoto kwa washambuliaji wengine wa Talaba kwani kwenye vinara wa ufungaji wawili kutoka kwenye chama hilo wameweka bao moja kila mmoja.

Anayeongoza kwa sasa ni Khalid Kofi wa Al Karkh mwenye mabao matano sawa na Temirov Sherzod wa Erbil.