ZIKIWA zimesalia siku sita tu kabla ya Simba kutupa karata ya kwanza katika mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Atletico ya Angola, kocha wa timu hiyo, Dimitar Pantev amewaambia mastaa wa timu hiyo anataka wafanye mambo yatakayowabeba kundini.
Hatua ya Pantev kuwapa wachezaji masharti hayo, imetokana na jinsi alivyovutiwa na timu hiyo ilivyocheza katika mechi ya kirafiki dhidi ya JKT Tanzania na kushinda kwa mabao 6-0, akisema anataka kazi hiyo iendelee hata kwa mechi zijazo za kimataifa ili Simba ikae pazuri.
Pantev anayetimiza siku 44 tangu atambulishwe rasmi na Simba Oktoba 3 mwaka huu akitokea Gaborone United ya Botswana, alisema anataka kuona Simba ikishambulia na kuzuia kwa pamoja bila kuruhusu mianya inayoweza kuwapa wapinzani nafasi ya kupenya kirahisi kwao.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo raia wa Bulgaria alisema kwa kiwango alichokiona katika ushindi wa 6-0 dhidi ya JKT Tanzania katika wiki ya kalenda ya FIFA kimempa tumaini kubwa la kufanikisha ndoto za Simba kufika mbali msimu huu, huku akisubiri kuungana na baadhi ya wachezaji ambao walikuwa katika majukumu ya timu za taifa.
“Huo mchezo (dhidi ya JKT) ulinipa picha halisi ya kile kikosi kinaweza kufanya. Tulishambulia kama timu na kuzuia pamoja, hatukutoa nafasi za wazi kwa wapinzani wetu. Huo ndio ufanisi ninaouhitaji katika kila mechi na hili ndio ambalo tumekuwa tukilifanyia kazi,” alisema Pantev.
Katika mashindano yote msimu huu, Simba imecheza mechi nane, imeshinda saba zikiwamo nne za raundi ya awali za Ligi ya Mabingwa, tatu za Ligi Kuu Bara na kupoteza pambano moja la Ngao ya Jamii mbele ya Yanga iliyoshinda kwa bao 1-0, huku Wekundu wa Msimbazi hao wakifunga mabao 13 na kuruhusu manne tu hadi sasa kuonyesha walivyo imara eneo la ulinzi.
Pantev, pia ameyataja mambo muhimu ambayo wachezaji hawapaswi kuyapuuza katika kipindi hiki kabla ya kuikaribisha Petro Atletico ni pamoja na heshima kwa kila mpinzani watakayekabiliana naye katika hatua hiyo ya makundi, hilo litawafanya kuwa salama.
Katika mazoezi yao, Simba inaelezwa imekuwa ikifanyia kazi muunganiko kati ya safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji, ili kuhakikisha inapopanda mbele pia wanapaswa kurudi na kulinda pamoja ili kuiweka katika nafasi nzuri ya kupata matokeo chanya kwa kila mechi uwanjani.
Hii ni moja ya vitu ambavyo meneja huyo amekuwa akifanyia kazi tangu akabidhiwe kijiti cha Fadlu Davids aliyehamia Raja Casablanca ya Morocco.
“Kushambulia bila ya muundo maalum ni hatari. Katika makundi ya CAF, ukifanya hivyo unajichimbia kaburi. Nataka kila mchezaji ajitoe kwenye matukio yote mawili katika muundo wetu yani tukiwa na mpira na bila ya mpira,” alisema Pantev.
Taarifa kutoka ndani ya kambi ya timu zinasema kocha huyo anayetambulishwa kama meneja amekuwa akitoa programu za mazoezi yenye kasi, umakini wa uamuzi wa haraka na kupanga safu mbili za ulinzi zinazosogea kwa uelewano. Mazoezi hayo ndiyo yaliyowasaidia dhidi ya JKT ambapo Simba ilionekana kuwa na nidhamu na uhai mkubwa wa kushambulia.
Katika eneo la kiungo, Pantev inaelezwa amempa majukumu mapya Alassane Kante kusimamia mabadiliko ya kasi, kuhakikisha timu inahamia mbele kwa pasi chache, lakini zenye uelekeo, huku Joshua Mutale, Charles Jean Ahoua, Ellie Mpanzu na viungo wengine washambuliaji, wakipewa majukumu ya kuwa injini ya kusukuma timu wakati wote.
Kwa upande wa safu ya ushambuliaji inaendelea kuimarika chini ya Jonathan Sowah ambaye katika mechi dhidi ya JKT alipachika mabao mawili, hivyo anategemewa kwamba atakuwa silaha muhimu kwa Pantev katika mechi ya Jumapili dhidi ya Petro Atletico.
Ikumbukwe kuwa Sowah ndiye aliyepachika bao la ushindi wa Simba katika mechi ya Ligi dhidi hao hao JKT Tanzania wakati Wekundu wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1 kabla ya kalenda ya FIFA na kuifanya timu hiyo kupata ushindi wa tatu mfululizo.
Baada ya kukipiga dhidi ya Petro, Simba ambayo ipo Kundi D, itakuwa na safari ya kwenda Mali kukabiliana na Stade Malien katika mechi ya pili ya hatua hiyo ambayo itakuwa kati ya Novemba 28-30 kisha kusubiri mapema mwakani kuvaana na Esperance ya Tunisia ‘back to back’.